Lugha Nyingine
Mkutano wa 63 wa AALCO wafunguliwa nchini Uganda ukijikita katika sheria ya kimataifa
Wawakilishi wa serikali, wataalam wa sheria na wanadiplomasia kutoka nchi 49 wanachama wa Jumuiya ya Mashauriano ya Kisheria ya Asia na Afrika (AALCO) wameanza kukutana jana Jumatatu nchini Uganda kwa ajili ya mkutano wa 63 wa mwaka ili kusukuma mbele ushirikiano katika masuala muhimu ya kisheria na kimataifa.
Katika hotuba ya Rais Yoweri Museveni wa Uganda, iliyotolewa kwa niaba yake na Spika wa Bunge la Uganda Anita Among kwenye ufunguzi wa mkutano huo wa siku tano mjini Kampala, amezihimiza Asia na Afrika kufanya kazi kwa mshikamano ili kulinda maslahi yao.
"Tunapokutana leo hii, tunakabiliana na dunia iliyojaa changamoto ambazo hazijawahi kushuhudiwa. Mabadiliko ya tabianchi yanatishia mifumo ya ikolojia na maisha. Migogoro na ukosefu wa usalama vinauweka majaribuni utulivu. Kukosekana kwa usawa wa kiuchumi kunatatiza jamii. Aidha, maendeleo ya kasi ya kiteknolojia, kuanzia Akili Mnemba hadi usalama wa mtandaoni, yanaibua maswali tata ya kisheria ambayo yanahitaji umakini wetu” amesema.
Amebainisha kuwa katika muktadha huo, jukumu la AALCO ni muhimu zaidi kuliko hapo awali.
Ameihimiza jumuiya hiyo, si tu kuitikia mambo mapya ya kisheria yanayotokea duniani bali pia kushiriki kuyatengeneza kulingana na vipaumbele kama vile maendeleo endelevu, uhuru na haki.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



