Israel yashambulia jengo la Hamas mjini Doha; mtoto wa kiongozi wa Hamas auawa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 10, 2025

Wafanyakazi wa usalama wakionekana karibu na eneo linaloshambuliwa na Israel mjini Doha, Qatar, Septemba 9, 2025. (Picha na Nikku/Xinhua)

Wafanyakazi wa usalama wakionekana karibu na eneo linaloshambuliwa na Israel mjini Doha, Qatar, Septemba 9, 2025. (Picha na Nikku/Xinhua)

DOHA/JERUSALEM - Israel ilianzisha shambulizi la anga ambalo halijawahi kushuhudiwa katika mji mkuu wa Qatar, Doha jana Jumanne, likilenga jengo linalotumiwa na maafisa waandamizi wa Hamas katika kile ambacho mamlaka za Israel zimekielezea kuwa ni jaribio la kuua viongozi wa kundi hilo.

Hamas imesema katika taarifa yake baadaye siku hiyo ya Jumanne jioni kwamba shambulizi hilo lilitokea wakati wajumbe wake wakijadili pendekezo jipya la kusimamisha mapigano lililowasilishwa na Rais Donald Trump wa Marekani ambapo kwa mujibu wa kundi hilo, timu ya mazungumzo imenusurika, lakini wengine sita wameuawa.

Kundi hilo limewataja Wapalestina waliouawa kuwa ni Jihad Lubad, mkurugenzi wa ofisi ya mjumbe wa ofisi ya siasa ya Hamas Khalil al-Hayya; Hammam al-Hayya, mtoto wa Khalil al-Hayya; na wasindikizaji Abdullah Abdulwahid, Moamen Hassouna, na Ahmed al-Mamlouk. Pia limethibitisha kifo cha Badr Saad Mohammed al-Humaidi, askari wa Kikosi cha Usalama wa Ndani cha Qatar.

Mamlaka za Israel hazikuthibitisha mara moja ni nani aliyeuawa lakini katika taarifa ya pamoja, Jeshi la Israel na shirika la usalama la Shin Bet vimesema shambulizi hilo lililenga viongozi wa Hamas "waliohusika moja kwa moja na mauaji ya Oktoba 7" na vilitumia "silaha na upelelezi za kulenga kwa usahihi" ili kupunguza madhara kwa raia.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amelielezea shambulizi hilo kuwa ni "operesheni wa kujitegemea kabisa ya Israeli."

"Israel imelianzisha, Israel imelitekeleza, na Israel inachukua wajibu kamili," amesema katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani White House, Karoline Leavitt aliwaambia waandishi wa habari baadaye siku hiyo kwamba utawala wa Trump ulitaarifiwa na Jeshi la Marekani kwamba Israel ilikuwa ikipiga maeneo ya Hamas, "ambayo kwa bahati mbaya sana, yanapatikana katika sehemu ya Doha, mji mkuu wa Qatar."

Leavitt amesema kuwa Trump "alimwelekeza mara moja Mjumbe Maalum Steve Witkoff kuifahamisha Qatar kuhusu shambulizi lililokuwa linakuja, jambo ambalo alilifanya."

Hata hivyo, Qatar imekanusha kuwa na ufahamu wa awali, ikiyaelezea madai hayo "yasiyo na msingi."

"Mawasiliano ya simu kutoka kwa afisa wa Marekani yalikuja wakati wa sauti ya milipuko iliyosababishwa na shambulizi hilo la Israel mjini Doha," msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar Majed bin Mohammed Al Ansari amesema katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X, akiongeza kwamba wizara hiyo imelaani shambulizi hilo ikilielezea kuwa ni "tishio kubwa" kwa raia na wakaazi, ukiukaji wa mamlaka, na imetangaza kusimamisha mazungumzo yanayoendelea.

Shambulizi hilo limesababisha lawama za kimataifa. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani shambulizi hilo akisema ni "ukiukaji wa wazi" wa mamlaka ya Qatar.

Saudi Arabia pia imekosoa kile ilichokielezea kuwa ni kuendelea kwa ukiukaji wa Israel katika eneo hilo, ikirejelea mashambulizi ya hivi karibuni katika majimbo ya Homs na Latakia ya Syria kuwa ni ukiukaji wa sheria za kimataifa na Makubaliano ya Kutoshambuliana ya mwaka 1974.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha