

Lugha Nyingine
Afrika Kusini kamwe "haitapiga goti" kwenye mazungumzo ya kibiashara na Marekani: Rais Ramaphosa
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini akijibu maswali kwenye Bunge la Taifa mjini Cape Town, Afrika Kusini, Septemba 9, 2025. (Picha na Xabiso Mkhabela/Xinhua)
CAPE TOWN - Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema kwamba serikali yake inazungumza na Marekani kwa juhudi ili kupata makubaliano ya haki ya biashara na uwekezaji, lakini akasisitiza kuwa nchi hiyo "haitapiga goti" katika mazungumzo hayo.
Akijibu maswali kwenye Bunge la Taifa jana Jumanne mchana mjini Cape Town, Rais Ramaphosa amewaambia wabunge kwamba wawakilishi wa serikali ya Afrika Kusini kwa sasa wako Marekani kwa mazungumzo rasmi zaidi.
"Watu wetu, ambao wako Marekani, sasa wako katika nguvu kamili na aina hii ya mkakati," amesema, akiongeza kuwa mawaziri wa biashara na viwanda na uhusiano wa kimataifa wataungana nao kuendeleza majadiliano.
“Wanakutana na wadau kadhaa wakiwemo wawakilishi katika utawala, wabunge, wadau wa biashara, na wengineo,” ameongeza.
Rais huyo amesema kuwa lengo la mazungumzo hayo yanayoendelea na Marekani ni kupata makubaliano ya kibiashara na uwekezaji ya kunufaishana, akiongeza kuwa serikali imechagua njia hiyo ya mazungumzo baada ya kushauriwa na wauzaji bidhaa nje, waagizaji bidhaa nje, vyama vya wafanyakazi na sekta binafsi.
"Chaguo letu linatokana na kile tunachotaka kupata. Na tunachotaka kupata ni kuendelea kuuza bidhaa Marekani nyingi kadri iwezekanavyo, na kuwezesha kampuni pia kuwekeza nchini Marekani, lakini pia kuwezesha kampuni za Marekani kuwekeza kwetu," Rais Ramaphosa amesema.
Wakati huo huo, rais huyo amesisitiza kuwa Afrika Kusini iliingia katika mazungumzo ikiwa na turufu kubwa, akirejelea utajiri wa madini na uwezo wa kuchakata wa nchi hiyo.
Rais Ramaphosa amekiri kwamba utawala wa Marekani wakati fulani unaweza kuwa "usiotabirika" na wa "kulipiza kisasi," lakini amesema ana imani kuwa mkakati wa mazungumzo utatoa matokeo chanya.
"Tumesema hatutaonewa. Tutasimama kama nchi huru na kujadiliana na kupata makubaliano bora zaidi kwa Afrika Kusini. Hilo ndilo hasa tunalofanya," amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma