China yaeleza kupinga hatua ya nchi tatu za Ulaya kuchukua hatua dhidi ya Iran, yatoa wito wa kuongeza juhudi za kidiplomasia

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 11, 2025

Picha iliyopigwa Septemba 10, 2025 ikionyesha mwonekano wa mkutano wa Baraza la Magavana wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) mjini Vienna, Austria. (Ujumbe wa Kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa na Mashirika mengine ya Kimataifa mjini Vienna/kupitia Xinhua)

Picha iliyopigwa Septemba 10, 2025 ikionyesha mwonekano wa mkutano wa Baraza la Magavana wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) mjini Vienna, Austria. (Picha inatoka Ujumbe wa Kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa na Mashirika mengine ya Kimataifa mjini Vienna/kupitia Xinhua)

VIENNA - China inapinga vikali hatua ya nchi tatu za Ulaya (E3) za Ufaransa, Uingereza na Ujerumani ya kutumia utaratibu wa haraka wa "snapback" wa kurejesha vikwazo dhidi ya Iran, na inatoa wito wa juhudi zaidi za kidiplomasia kuhusu suala la nyuklia la Iran, mjumbe wa kudumu wa China katika Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), Li Song amesema jana Jumatano kwenye mkutano wa Bodi ya Magavana wa IAEA, akisema hatua ya namna hiyo haitasaidia kujenga tena hali ya kuaminiana na kurejea katika mazungumzo, badala yake inaweza kusababisha matokeo mabaya na kuharibu juhudi za kidiplomasia.

"Suala la nyuklia la Iran linaweza tu kutatuliwa ipasavyo kwa msingi wa kuheshimu kikamilifu haki ya Iran ya matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia, kuhakikisha hali ya amani kwa mpango wa nyuklia wa Iran, na iliyoongezewa ukaguzi mkali wa kimataifa chini ya mfumo wa IAEA," Li amesema.

Agosti 28, nchi hizo tatu zililiarifu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) kwamba zilikuwa zimeanzisha utaratibu huo chini ya makubaliano ya nyuklia ya Iran ya 2015, ukiongeza uwezekano wa kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran katika siku 30.

Li pia amesema kuwa mwezi Juni mwaka huu, Marekani na Israel zilianzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran vilivyo chini ya ulinzi wa IAEA, hali ambayo ilidhoofisha sana juhudi za kidiplomasia juu ya suala hilo la nyuklia la Iran na kuingilia kwa kiasi kikubwa ushirikiano wa ulinzi kati ya Iran na IAEA.

"China inapinga vikali uonevu wa umwamba na inazitaka Marekani na Israel zisitumie vibaya nguvu za kijeshi," Li amesema.

Mjumbe huyo wa China amesema China itaendelea kushirikiana na pande zote kwa namna ya kikanuni, uwajibikaji na kiujenzi ili kuurudisha mchakato wa kisiasa na kidiplomasia wa suala hilo la nyuklia la Iran, na kulinda kithabiti utaratibu wa kimataifa wa kutoeneza silaha za nyuklia.

Utaratibu huo wa "snapback" ni kifungu katika makubaliano ya nyuklia ya 2015 kati ya Iran na nchi zenye nguvu duniani ambacho kinaruhusu pande nyingine kuweka tena vikwazo vyote vya kimataifa kama Iran itashindwa kuzingatia makubaliano hayo.

Iran ilitia saini makubaliano ya nyuklia, ambayo yanajulikana rasmi kama Mpango wa Kina wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA), mwaka 2015 na nchi sita - Uingereza, China, Ufaransa, Ujerumani, Russia na Marekani. Chini ya makubaliano hayo, Tehran ilikubali kuzuia mpango wake wa nyuklia ili kubadilishana na kupungua kwa vikwazo.

Marekani ilijiondoa kwa upande mmoja katika makubaliano hayo mwaka 2018 na kurejesha vikwazo hivyo, hali ambayo iliifanya Iran kupunguza hatua kwa hatua kufuata ahadi zake za nyuklia.

Li Song, Mjumbe wa Kudumu wa China katika IAEA, akihutubia mkutano wa Baraza la Magavana wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) mjini Vienna, Austria, Septemba 10, 2025. (Ujumbe wa Kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa na Mashirika mengine ya Kimataifa mjini Vienna/kupitia Xinhua)

Li Song, Mjumbe wa Kudumu wa China katika IAEA, akihutubia mkutano wa Baraza la Magavana wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) mjini Vienna, Austria, Septemba 10, 2025. (Picha inatoka Ujumbe wa Kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa na Mashirika mengine ya Kimataifa mjini Vienna/kupitia Xinhua)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha