Nchi za kikanda zasisitiza tena lawama zao juu ya shambulizi la Israel mjini Doha huku Israel ikiapa kutafuta viongozi wa Hamas "kila mahali"

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 11, 2025

Mfalme Abdullah II wa Jordan (katikati) akikutana na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina (wa pili kushoto) aliyeko ziarani mjini Amman, Jordan, Septemba 10, 2025. (Kasri la Kifalme la Hashemite/kupitia Xinhua)

Mfalme Abdullah II wa Jordan (katikati) akikutana na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina (wa pili kushoto) aliyeko ziarani mjini Amman, Jordan, Septemba 10, 2025. (Kasri la Kifalme la Hashemite/kupitia Xinhua)

CAIRO - Nchi za kikanda zimesisitiza tena lawama zao juu ya shambulizi la Israel mjini Doha, na kuelezea uungaji mkono na mshikamano wao na Qatar, huku maafisa wa Israel wakiapa kuendelea kupambana na viongozi wa Hamas "kila mahali" na kulenga nchi zinazoshindwa kuchukua hatua dhidi yao.

Juzi Jumanne, Israel ilianzisha shambulizi la anga ambalo halijawahi kushuhudiwa katika mji mkuu wa Qatar, Doha, likilenga jengo linalotumiwa na maafisa waandamizi wa Hamas katika kile ambacho mamlaka za Israel zilikielezea kuwa ni jaribio la kuua viongozi wa kundi hilo ambao "walihusika moja kwa moja" na shambulizi la Oktoba 7, 2023 ambalo lilisababisha vifo vya watu takriban 1,200.

Hamas ilisema baadaye kuwa shambulizi hilo lilitokea wakati wajumbe wake wakijadili pendekezo jipya la kusimamisha mapigano lililowasilishwa na Marekani ambapo kundi hilo lilisema timu ya mazungumzo imenusurika, lakini wengine sita wameuawa.

Siku hiyohiyo ya Jumanne jioni, Qatar ilisema itachukua mbinu "ya kina" kujibu shambulizi hilo la Israel na kuzuia mashambulizi ya siku za baadaye, ikiongeza kuwa nchi hiyo haitavumilia hatua yoyote ya kukiuka mamlaka yake.

Hata hivyo, Qatar imetoa hakikisho tena kuwa upatanishi wa kusimamisha mapigano na kubadilishana wafungwa huko Gaza vitaendelea.

Jana Jumatano, Waziri wa Ulinzi wa Israel Israel Katz alisema shambulizi hilo la Doha ni sehemu ya operesheni iliyopewa jina la "Kilele cha Moto" inayolenga kuwaua viongozi wa juu wa Hamas.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameonya kwamba nchi zinazokuwa wenyeji wa viongozi wa Hamas au makundi mengine yanayochukuliwa na Israel kama maadui zinaweza zenyewe kulengwa iwapo zitashindwa kuchukua hatua dhidi yao.

Huku kukiwa na mwenendo huo mpya wa mambo, Sheikh Abdullah bin Zayed Al Nahyan, naibu waziri mkuu na waziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), amesema kwenye mkutano na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Badr Abdelatty mjini Abu Dhabi kwamba UAE inaunga mkono hatua zote ambazo Qatar inaweza kuchukua ili kuhakikisha ulinzi na usalama wake.

Katika mazungumzo ya simu siku ya Jumatano kati ya Rais Abdel-Fattah al-Sisi wa Misri na Amir wa Kuwait Sheikh Meshal Al-Ahmad Al-Jaber Al-Sabah, viongozi hao wawili wameelezea "mshikamano kamili" na Qatar, na kulielezea shambulizi hilo la Israel kuwa ni uingiliaji usiokubalika dhidi ya mamlaka ya Qatar.

Kwenye mkutano wake na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina mjini Amman jana Jumatano, Mfalme Abdullah II wa Jordan amelaani shambulizi hilo la Israel mjini Doha, kukataa mipango ya Israel ya kupanua udhibiti wa Gaza na shughuli za makazi katika Ukingo wa Magharibi, amesisitiza haja ya kusimamisha mapigano huko Gaza na ufikiaji usiozuiliwa wa kibinadamu, na utekelezaji wa suluhu ya nchi mbili, taarifa ya Kasri la Kifalme imeeleza.

Mfalme Abdullah II wa Jordan (kulia) akishikana mikono na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina aliyeko ziarani mjini Amman, Jordan, Septemba 10, 2025. (Kasri la Kifalme la Hashemite/kupitia Xinhua)

Mfalme Abdullah II wa Jordan (kulia) akishikana mikono na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina aliyeko ziarani mjini Amman, Jordan, Septemba 10, 2025. (Kasri la Kifalme la Hashemite/kupitia Xinhua)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha