Watu zaidi ya 80 wauawa katika mashambulizi ya waasi mashariki mwa DRC

(CRI Online) Septemba 11, 2025

Watu zaidi ya 80 wameuawa katika mashambulizi mfululizo yaliyofanywa na waasi wa Allied Democratic Forces (ADF) mashariki mwa DRC, serikali ya DRC imesema, huku Umoja wa Afrika (AU) ukilaani shambulizi hilo baya la kigaidi.

Kwa mujibu wa taarifa ya jimbo iliyorejelewa katika taarifa hiyo ya serikali ya DRC, watu angalau 71 wameuawa na wengine kadhaa hawajulikani walipo baada ya shambulizi la ADF huko Ntoyo katika eneo la Lubero Jimbo la Kivu Kaskazini.

Afisa Tawala wa Lubero Kanali Alain Kiwewa ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kwamba idadi ya vifo imeongezeka hadi kufikia zaidi ya 80.

Katika taarifa yake, Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU Mahmoud Ali Youssouf amelaani vikali shambulizi hilo la Ntoyo na ghasia za mara kwa mara zinazolenga raia mashariki mwa DRC.

Amesisitiza tena dhamira ya AU katika kuunga mkono juhudi za kitaifa, kikanda na kimataifa kurejesha amani, usalama na utulivu katika eneo la Maziwa Makuu.

Serikali ya DRC imesisitiza tena azma yake ya kuongeza juhudi za kulinda raia, kurejesha usalama, na kufanya kazi na washirika kukomesha operesheni za kijeshi za ADF.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha