

Lugha Nyingine
China yazindua mpango wa mafunzo ya huduma ya kwanza kwenye eneo la tukio nchini Sierra Leone
Daktari wa timu ya 26 ya madaktari wa China nchini Sierra Leone akiwaelekeza wanagenzi wenyeji katika mafunzo ya ufufuaji wa moyo na mapafu (CPR) mjini Freetown, Sierra Leone, Septemba 10, 2025. (Picha inatoka timu ya 26 ya madaktari wa China nchini Sierra Leone/kupitia Xinhua)
FREETOWN - Kituo cha kwanza cha Mafunzo ya Huduma ya Kwanza kwenye Eneo la Tukio cha Sierra Leone-China kimezinduliwa rasmi Jumatano wiki hii katika Hospitali ya Urafiki kati ya Sierra Leone na China huko Freetown, mji mkuu wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Kituo hicho cha mafunzo kinalenga kuwapa mafunzo wananchi wa Sierra Leone katika huduma za matibabu ya dharura, na kuwapa ujuzi ambao ni muhimu katika kushughulikia hali za huduma ya kwanza ipasavyo.
"Kituo hiki kimefungua ukurasa mpya katika ushirikiano wetu na Sierra Leone," amesema Liu Longfei, mkuu wa timu ya 26 ya madaktari wa China nchini Sierra Leone, akisisitiza dhamira ya timu hiyo ya madaktari kwa afya na usalama wa wenyeji.
Timu hiyo ya madaktari, ikiwa mwanzilishi mkuu wa kituo hicho cha mafunzo, inalenga kusukuma mbele na kuvumbua mafunzo ya huduma ya kwanza kwenye eneo la tukio huku ikichangia utaalamu wa China kwenye mfumo wa afya wa Sierra Leone.
Balozi wa China nchini Sierra Leone Wang Qing amesema kuwa timu hiyo ya madaktari kutoka Mkoa wa Hunan imekuwa ikijishughulisha na kazi mbalimbali zenye mafanikio za matibabu na mafunzo kwa wahudumu wa afya katika miaka mingi iliyopita.
"Kituo hiki kitasaidia kuleta huduma zaidi za matibabu karibu na jamii," amesema.
Sartie Kanneh, ofisa mkuu wa matibabu wa Wizara ya Afya ya Sierra Leone, amesisitiza lengo la pamoja kati ya juhudi za wizara hiyo na juhudi za China za kuhimiza maendeleo ya sekta ya afya nchini Sierra Leone.
Amesema uungaji mkono wa kihistoria kutoka kwa China katika nyakati ngumu, zikiwemo za mlipuko wa Ebola, COVID-19, na milipuko ya hivi karibuni ya ugonjwa wa mpox.
"Tunafurahi kuwa na kituo hiki cha kwanza cha huduma ya kwanza kwenye eneo la tukio ambacho kitapunguza changamoto nyingi ambazo watu wanakabiliana nazo kwa sasa linapokuja suala la matibabu ya dharura," Kanneh amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma