Miaka mitatu mfululizo ya kutembelea Shenzhen, China nabaki kuduwazwa kwa maendeleo na mageuzi yake ya kila wakati

By Aris (Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 28, 2025

C:\Users\Aris\xwechat_files\wxid_v8myaetwua8l22_09e2\temp\RWTemp\2025-09\5879ca9650744b22f0107e95d023b75b.jpg

Picha ikionesha maghorofa ya usanifu wa siku za baadaye mjini Shenzhen, China. (Picha/People's Daily Online)

Nimepata kuutembelea mji wa Shenzhen, China kwa mara ya tatu sasa kwa miaka mitatu mfululizo, 2023, 2024 na sasa mwaka huu wa 2025. Jambo moja ambalo ni dhahiri ni kwamba, kila ninapoutembelea mji huo “kijana” wa China wenye kubeba uhai na mustakabali wa dunia kutokana na kushamiri uvumbuzi wa sasa na wa siku za baadaye, huwa nakuta umebadilika sana na kuwa na taswira mpya kabisa.

Ninaweza kusema kwa hakika kwamba, Shenzhen hubadilika kila sekunde, kila dakika, kila saa, kila siku na na kila mwaka. Na huu ndiyo msingi wenyewe wa mji huo kuwa kitovu cha uvumbuzi wa teknolojia nyingi za hali ya juu na akili mnemba, ukivutia vijana na kampuni bora kutoka kila kona ya dunia kuja kuweka makazi na kutimiza ndoto zao.

Tangu nilipokanyaga Shenzhen mwaka 2023 kwa mara ya kwanza, pamoja na kukaa kwa takribani wiki nzima, fikra na hisia za mwili vilikuwa vikinigomea kuondoka, macho yalikuwa bado yana “njaa” ya kutazama, kuduwaa na kuyaishi maendeleo yasiyo ya kawaida ya mji huo. Nililazimika kuondoka nikiwa na mpango kichwani wa kurudi Shenzhen mapema iwezekavyo.

Hakika, nilifanya hivyo, mwaka 2024 tena nilirudi tena Shenzhen kwa safari binafsi, nikiwa na lengo kichwani la kukata kiu hiyo. Kuanzia kushangaa huduma za kiotomatiki katika maeneo mbalimbali, usafi wa kiwango cha taka-sifuri mjini, majengo ya kipekee yenye usanifu wa siku za baadaye, hadi miundombinu ya usafiri yenye kiwango kisichoelezeka, mji uliopangiliwa kama picha za kuchorwa na vyakula vitamu vya baharini vinavyomtoa mtu mate muda wote, bado niliondoka nikiwa na kiu ya Shenzhen.

Hatimaye mwaka huu wa 2025, umetimiza miaka mitatu mfululizo ya mimi kutembelea Shenzhen. Septemba 14 nikiwa na timu ya waandishi wa habari wenzangu wa People's Daily Online, tulifunga safari. Safari ambayo ninaweza kuielezea kuwa ni sehemu ya mwendelezo wa ndoto na mpango wangu wa kuitazama na kuifahamu Shenzhen ingawa muda wote nimekuwa nikibaki kuduwazwa na uzuri na mng'aro wake wa kipekee unaobadilika kila wakati.

Katika safari hii, nayo pia kama kawaida nimekuta Shenzhen ya tofauti, iliyobadilika sana kuliko mwaka jana na ule wa juzi. Nimeikuta Shenzhen ikiwa imebeba miradi na mipango kabambe, mipya, ya mwendelezo na yenye kupanua maono yaliyokuwepo kuwa makubwa zaidi. Nimeikuta Shenzhen ambayo si tu inaendelea kudhihirisha kwa vitendo maana halisi ya kuwa mji wa kisasa wa kiteknolojia lakini pia mji wenye kubeba mustakabali wa dunia yetu.

C:\Users\Aris\xwechat_files\wxid_v8myaetwua8l22_09e2\temp\RWTemp\2025-09\1debbfbe3ace8a82a7a4ccbec1dbba8f.jpg

Picha ikionesha Kituo cha Uvumbuzi cha Vijana cha Qianhai Shenzhen Hong Kong mjini Shenzhen, China. (Picha/People's Daily Online)

Kwenye ziara katika Eneo Maalum la Ushirikiano la Qianhai, nilitembelea Kituo cha Uvumbuzi cha Vijana cha Qianhai Shenzhen Hong Kong ambako nilishuhudia namna serikali ya Mji wa Shenzhen inavyojenga mazingira ya kuzalisha, kulea na kuendeleza uvumbuzi, vipaji na kampuni za kiteknolojia. Hali ambayo si tu inaleta uvumbuzi wa nguvu mpya za uzalishaji zenye sifa bora bali pia inajenga jukwaa la uzalishaji lenye ushawishi kimataifa na kutimiza ndoto za vijana wengi kutoka nchi na maeneo mbalimbali duniani.

C:\Users\Aris\xwechat_files\wxid_v8myaetwua8l22_09e2\temp\RWTemp\2025-09\a0e528cdb5f4a9a46d5e170fb1f540e3.jpg

Roboti ya muundo wa binadamu ikibeba mizigo kwenye moja ya kampuni mjini Shenzhen, China. (Picha/People’s Daily Online)

Shenzhen, ambayo ni mji mtangulizi wa sera za mageuzi na ufunguaji mlango na baadaye ile ya kwenda kimataifa za China, si tu inaendelea kuziishi sera hizo, bali pia imezitumia kuwa lango la kudumu la China kwa Dunia. Mathalani, nikiwa kwenye Kituo cha Mtandaoni cha Biashara ya Kimataifa cha Qianhai, nimeshuhudia namna Shenzhen, kupitia mamlaka za Qianhai, inavyojenga jukwaa linalotafuta kuifanya Qianhai kuwa eneo la hadhi ya juu kwa kampuni za China zinazotafuta kupanua biashara zao ng'ambo. Kituo hicho, hutoa huduma jumuishi mtandaoni na nje ya mtandaoni zote katika sehemu moja kwa hatua zote nne za kampuni za China kupanua uwepo wao ng'ambo: kupanga mipango ya awali, mipangilio ya maandalizi, uendeshaji kwenye eneo la mradi na maendeleo salama.

Juhudi hizo za kuwezesha kampuni za China kupanua shughuli zao ng'ambo zipo pia katika kituo cha huduma za kimataifa kwa kampuni za China kwenda kimataifa. Katika kituo hiki, nimeshuhudia namna kinavyofanya kazi ya kuwa makao makuu ya kampuni za China zinazopanua uwepo wao kimataifa wakati huohuo kikitoa lango la kimkakati kwa kampuni za kigeni zinazoingia katika soko la China.

C:\Users\Aris\xwechat_files\wxid_v8myaetwua8l22_09e2\temp\RWTemp\2025-09\0e033eb2d40b0e651f876ea202ccaae2.jpg

Picha ikionesha majengo ya maghorofa mjini Shenzhen, China. (Picha/People’s Daily Online)

Kufungua mlango na kuwezesha kampuni za China kupanua shughuli zao kimataifa lazima kwende sambamba na kuwezesha miamala na mabadilishano ya kuvuka mpaka. Mji wa Shenzhen, kupitia Kituo cha Usimamizi Uchukuzi wa Bidhaa za Biashara ya Kuvuka Mpaka cha Shenzhen unafanya hasa hilo. Kituo hicho kimejenga mifumo ya teknolojia mahiri za kisasa ya kufuatilia na kuidhinisha bidhaa na malori yenye kubeba bidhaa hizo ili kuziharakisha kwenda kwenye masoko ya kimataifa. Kituo hiki si tu kimekuwa nguzo muhimu ya biashara ya kuvuka mpaka ya Eneo la Ghuba Kuu ya Guangdong-Hong Kong-Macao bali pia kimeifanya Shenzhen kuwa lango la kupitisha na kuingiza bidhaa kutoka na kuingia China kuptia biashara ya kuvuka mpaka.

C:\Users\Aris\xwechat_files\wxid_v8myaetwua8l22_09e2\temp\RWTemp\2025-09\5e45e7ee9f7ff893deaf28165a8a2b5b.jpg

Roboti ya muundo wa binadamu ikifanya kazi kwenye moja ya kampuni mjini Shenzhen, China. (Picha/People’s Daily Online)

Uvumbuzi wa kisayansi na kiteknolojia na dhana nzima ya mji wa kisasa wenye kuendeshwa na teknolojia za hali ya juu na akili mnemba (AI) katika karibu nyanja zote, ni vitu vinavyoitambulisha Shenzhen. Katika pitapita zangu mtaani na kutembelea maeneo ya huduma na miradi ya sayansi na teknolojia, naweza kusema kwa hakika kabisa, nimeshuhudia Shenzhen yenye uchumi wa maarifa na wa kiotomatiki, isiyotegemea kabisa miamala taslimu, yenye maghorofa marefu ya usanifu wa siku za baadaye, mifumo ya usafiri wa umma ambayo haitegemei binadamu na zaidi, yenye mageuzi makubwa na ya kasi katika China iliyojaa uvumbuzi.

Moja ya mambo yaliyonivutia kipekee ni kuanzishwa kwa mji wa sayansi wa Guangming, kituo cha kisayansi na kiteknolojia kilichojengwa kwenye eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 99, kikiwa na malengo ya kuja kuwa mji wa kisayansi wa kiwango cha daraja la kwanza duniani ifikapo mwaka 2035. Kwa mujibu wa maelezo tuliyopewa, ndani ya mji huo kutakuwa na vituo vikubwa vya kisayansi na taasisi za utafiti katika maeneo kama vile sayansi ya ubongo, baiolojia ya sintetiki, na nyenzo mpya, zikilenga kuendeleza uvumbuzi na kuufanya mji huo kuwa kituo kikuu cha kitaifa cha sayansi cha China.

C:\Users\Aris\xwechat_files\wxid_v8myaetwua8l22_09e2\temp\RWTemp\2025-09\55b3016f8365b36eab270f2e13a0a43c.jpg

Picha ikionyesha mwonekano wa nje ya Jumba la Makumbusho ya Sayansi na Teknlojia la Shenzhen, China. (Picha/People's Daily Online)

Nimeweza kushuhudia mafanikio makubwa na dhahiri kuelekea kutekeleza mpango huo kapambe wa mji wa sayansi wa Guangming. Moja ya miradi yake kinara ni Jumba la Makumbusho ya Sayansi na Teknolojia la Shenzhen ambalo mbali na kusanifiwa kwa muundo wa siku za baadaye wa umbo la anga ya juu, ndani yake limesheheni vitu mbalimbali vinavyoakisi hatua mbalimbali za maendeleo ya sayansi na teknolojia kuanzia teknolojia za mawasiliano, roboti za muundo wa binadamu za kutoa huduma hadi vifaa changamani vya kuwasiliana na kufanya michezo mbalimbali kwa kushirikiana na binadamu.

Ndani yake nilihudumiwa kahawa na roboti kuanzia kuiandaa hadi kunikabidhi mkononi. Niliweza kucheza michezo kama vile soka, tenisi ya mezani, mpira wa kikabu na hata kucheza muziki na roboti. Nikiwa ndani yake nilihisi niko ulimwengu mwingine kabisa, ambao ninaweza kuishi nikiwa na "rafiki zangu binadamu roboti".

C:\Users\Aris\xwechat_files\wxid_v8myaetwua8l22_09e2\temp\RWTemp\2025-09\b6d9df11e78984ab0a996a765dcc4e9a.jpg

Watalii wa kigeni wakiwa katika Mji wa Kale wa Nantou mjini Shenzhen, China. (Picha/People’s Daily Online)

Jambo lingine la kipekee lililonivutia ni mjumuiko wa mambo ya kisasa na yale ya kale na ya kijadi. Kwa mgeni anayefika Shenzhen kwa mara ya kwanza na kuduwazwa na maendeleo na maghorofa yake marefu yenye kugusa anga anaweza kudhani, mji huo hauna mambo mazuri ya kale yenye kuonesha historia, jadi, tamaduni na mchanganyo wa usasa na ukale.

Nilipofika Mji wa Kale wa Nantou, unaojulikana pia kwa jina la Mji Mkongwe wa Xin'an niliweza kuona namna unavyowakilisha mizizi ya kitamaduni ya Shenzhen na Hong Kong ukiwa na mchanganyiko wa kipekee wa historia, mila, na uhuishaji upya wa kisasa wa miji. Mji huo mkongwe wenye umri wa miaka zaidi ya 1,700 katika Wilaya ya Nanshan yenye maendeleo ya kisasa, unaionesha Shenzhen ya tofauti, yenye kuchanganya ukale na usasa, ikiwapa vijana wa kisasa urithi kutoka zama za nyuma.

C:\Users\Aris\xwechat_files\wxid_v8myaetwua8l22_09e2\temp\RWTemp\2025-09\df9c0e29f43a7e697d9b1a9e737664fb.jpg

Kifaa cha teknolojia za kisasa cha kufagia mtaani kikionekana mjini Shenzhen, China. (Picha/ People’s Daily Online)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha