Lugha Nyingine
Afrika Kusini yachaguliwa tena kwenye baraza la usafiri wa anga duniani la UN
Wizara ya Uchukuzi ya Afrika Kusini imetangaza jana Jumapili kuwa Afrika Kusini imechaguliwa tena katika Baraza la Uongozi la Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara hiyo, uchaguzi huo ulifanyika Jumamosi kwenye Mkutano Mkuu wa 42 wa ICAO unaoendelea mjini Montreal, Canada, ambapo Afrika Kusini imetetea nafasi yake katika Sehemu ya II ya baraza hilo, kitengo ambacho kinawapa nchi wanachama uwakilishi wa juu katika majukwaa ya usafiri wa anga ya kimataifa.
Katika taarifa hiyo, Waziri wa Uchukuzi wa Afrika Kusini, Barbara Creecy amekaribisha matokeo hayo, akisema yanathibitisha tena mamlaka ambayo Afrika Kusini imekuwa ikiyashikilia tangu 2003 na inaonesha imani ya nchi wanachama kwa nchi hiyo na mchango wake unaoendelea katika kuunda ajenda ya kimataifa ya usafiri wa anga.
Mkutano wa 42 wa ICAO, wenye kaulimbiu "Anga Salama, Mustakabali Endelevu," unaendelea hadi Oktoba 3 na unawaleta pamoja nchi wanachama wote 193 ili kuamua kuhusu sera za anga za kimataifa, kuchagua wajumbe wa baraza, na kupitia kazi ya shirika hilo katika nyanja za kiufundi, kisheria na kimazingira.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



