Lugha Nyingine
Watu saba wafariki katika mlipuko wa homa ya Bonde la Ufa nchini Senegal
Waziri wa Afya na Mambo ya Umma wa Senegal Dkt. Ibrahima Sy ametangaza kwamba mlipuko wa hivi karibuni wa homa ya Bonde la Ufa (RVF) katika Mkoa wa Saint-Louis kaskazini mwa Senegal, umesababisha vifo vya watu saba huku 21 wakithibitishwa kuambukizwa.
Akiongoza mkutano kuhusu janga hilo katika eneo la Saint-Louis, Ibrahima Sy amesema kuwa mamlaka ya afya ya Senegal inashirikiana na mamlaka ya ufugaji wa wanyama kutekeleza kwa dhati hatua za kinga na udhibiti ili kuzuia kuenea zaidi kwa homa hiyo.
Mambukizi ya virusi vya RVF yaliripotiwa rasmi katika mkoa huo wa Saint-Louis tarehe 25 mwezi huu.
Mkuu wa Ufuatiliaji wa Maambukizi na Udhibiti wa Magonjwa (Epidemiological) katika Wizara ya Afya na Mambo ya Umma ya Senegal Boly Diop ameelezea kuwa RVF ni ugonjwa wa wanyama unaosababishwa na virusi vya homa ya Rift Valley. Amesema, kimsingi ugonjwa huo huenezwa kati ya wanyama, lakini wanadamu pia wanaweza kuambukizwa.
Ameeleza kuwa, wagonjwa kawaida hupata dalili kama vile homa, maumivu ya kichwa na misuli, na uchovu. Ameongeza kwamba, ingawa watu wengi walioambukizwa wana dalili ndogo, lakini kama hawatatibiwa wanaweza kuwa na matatizo ya kutokwa damu na kuhatarisha maisha yao.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



