China yahimiza nchi wanachama wa Kundi la Marafiki Wasioegemea upande wowote kufanyia mageuzi na kuboresha utawala duniani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 09, 2025

BEIJING - Zhao Leji, Spika wa Bunge la Umma la China, jana Jumatano ametoa wito kwa nchi wanachama wa Kundi la Marafiki Wasioegemea upande wowote kufanya kazi pamoja kuimarisha mfumo wa pande nyingi, na kuufanyia mageuzi na kuboresha utawala duniani.

Zhao, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Umma la China, ametoa wito huo katika hotuba yake kwa njia ya video aliyoitoa kwenye mkutano wa pili wa viongozi wa mabunge ya nchi wanachama wa Kundi la Marafiki Wasioegemea upande wowote, kwa mwaliko wa Dunyagozel Gulmanova, mwenyekiti wa Bunge la Taifa (Mejlis) la Turkmenistan.

"Tangu kuanzishwa kwake zaidi ya miaka mitano iliyopita, Kundi la Marafiki Wasioegemea upande wowote limekuwa jukwaa zuri kwa nchi wanachama wake kuongeza maelewano na hali ya kuaminiana, kuzidisha mawasiliano na ushirikiano, na kutekeleza mfumo wa pande nyingi," Zhao amesema.

Amesema kuwa mwaka huu ni maadhimisho ya miaka 80 tangu kupatikana ushindi katika Vita vya Dunia vya Kupinga Ufashisti na kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa (UN). Na kwamba, kwa vile dunia imeingia katika kipindi cha misukosuko na mageuzi, Umoja wa Mataifa na mfumo wa pande nyingi sasa vinakabiliwa na changamoto.

Zhao amesema kuwa mwanzoni mwa mwezi Septemba, Rais Xi Jinping wa China alitoa Pendekezo la Usimamizi Duniani (GGI), ambalo linasisitiza kanuni za usawa wa mamlaka, utawala wa sheria wa kimataifa, mfumo wa pande nyingi, mbinu ya utawala inayowapa kipaumbele watu, na hatua halisi.

"GGI -- inayolenga kuhimiza mfumo wa usimamizi duniani ulio wa haki na usawa zaidi -- ni pendekezo lingine kubwa, lililokaribishwa na nchi nyingi kufuatia Pendekezo la Maendeleo Duniani, Pendekezo la Usalama Duniani na Pendekezo la Ustaarabu Duniani," amesema.

Amesema, mkutano huo wa Jumatano wa viongozi wa mabunge umefuatilia zaidi mchango wa mazungumzo kati ya mabunge katika kulinda amani na kuaminiana duniani, na unabeba umuhimu mkubwa.

“Vyombo vya kutunga sheria vinabeba wajibu wa kusukuma mbele kikamilifu utawala duniani ulio wa haki, usawa, na kujenga jumuiya ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja,” ameongeza.

Ametoa wito kwa pande zote kutekeleza mapendekezo hayo manne duniani, kuimarisha ushirikiano, kuhuisha mfumo wa pande nyingi, kuufanyia mageuzi na kuboresha usimamizi duniani, na kithabiti kushikilia mfumo wa kimataifa huku Umoja wa Mataifa ukiwa ndiyo msingi wake na utaratibu wa kimataifa unaozingatia sheria za kimataifa.

Kundi hilo la Marafiki Wasiogemea upande wowote lilianzishwa mwezi Agosti 2020 kwa kupendekezwa na Turkmenistan. China ni miongoni mwa nchi wanachama waanzilishi 18.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha