Lugha Nyingine
Serbia yazindua huduma ya treni yenye ratiba ya kudumu kwenye reli iliyojengwa na Kampuni za China

Wahudumu wa treni wakisubiri abiria kupanda treni ya reli ya mwendo kasi ya Theungary-Serbia, mjini Belgrade, Serbia, Oktoba 3, 2025. (Picha na Wang Wei/Xinhua)
BELGRADE - Serbia imezindua huduma za treni za mwendo kasi zenye ratiba ya kudumu kati ya Belgrade na Subotica jana Jumatano, ikimaanisha kuanza kufanya kazi kikamilifu kwenye njia hiyo ya kwanza ya reli yenye kasi ya kilomita 200 kwa saa, mradi wa kihistoria chini ya Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja (BRI) lililopendekezwa na China.
Ikiwa inaendeshwa na kampuni ya taifa ya reli ya Serbia, Srbijavoz, sehemu ya Serbia yenye urefu wa kilomita 183.1 ya reli ya Hungary-Serbia inaunganisha mji mkuu, Belgrade na kaskazini mwa nchi hiyo. Treni hiyo ya Kati ya Mji sasa inakamilisha njia hiyo katika muda wa dakika 79 tu, ikipunguza muda wa kusafiri kutoka saa zaidi ya tano kabla ya kuboreshwa.
Treni ya kwanza ya mwendo kasi iliondoka katika Stesheni ya Belgrade mchana, ikiwa imebeba abiria 253. Katika kipindi cha siku tano cha ofa (Oktoba 8-12), abiria wanaweza kusafiri bila malipo.
Ikiwa imejengwa na Kampuni ya Kimataifa ya Reli ya China na Kampuni ya Ujenzi wa Mawasiliano ya China (CCCC), njia hiyo ya reli inatarajiwa kuchochea utalii, kuvutia uwekezaji na kuimarisha mafungamano ya mawasiliano ya kikanda.
Mapema mwezi huu, sehemu ya umbali wa kilomita 108 ya reli hiyo kutoka Novi Sad hadi Subotica ilikamilika. Sehemu ya Belgrade hadi Novi Sad imekuwa ikifanya kazi tangu Machi 2022.
Reli hiyo ya Hungary-Serbia yenye urefu wa kilomita 341.7, huku urefu wa kilomita 183.1 ukipitia Serbia, inawakilisha hatua kubwa katika ushirikiano wa reli kati ya China na Ulaya.

Rais wa Serbia Aleksandar Vucic akiangalia ubao kionyeshi wa reli ya mwendo kasi ya Hungary-Serbia mjini Subotica, Serbia, Oktoba 3, 2025.(Xinhua/Shi Zhongyu)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



