

Lugha Nyingine
Senegal yaandaa Jukwaa la kuvutia wawekezaji duniani
Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi wa Jukwaa la Wekeza nchini Senegal 2025 mjini Diamniadio, Senegal, Oktoba 7, 2025. (Ikulu ya Rais wa Senegal/kupitia Xinhua)
DAKAR – Jukwaa la Wekeza nchini Senegal 2025 limefunguliwa Jumanne wiki hii katika jiji la Diamniadio, karibu na mji mkuu wa Senegal, Dakar, likilenga kuharakisha uingiaji wa mtaji wa kigeni nchini humo.
Jukwaa hilo la siku mbili, chini ya kaulimbiu "Kuunganisha Fursa, Kujenga Mustakabali wa Siku za Baadaye," lilileta pamoja maafisa wa serikali, wataalam na wawekezaji wa kimataifa kutoka nchi mbalimbali.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye amesema nchi yake inafurahia faida bora nyingi katika kuvutia uwekezaji wa kigeni, akiongeza kuwa serikali bado ina dhamira ya kuboresha mazingira ya biashara na inakaribisha washirika kutoka sekta zote kunufaisha uzoefu na kujenga ushirikiano wa kunufaishana.
Kwenye jukwaa hilo, Rais Faye na Waziri Mkuu Ousmane Sonko walitembelea eneo la maonyesho la kampuni za China kwa mwaliko wa Balozi wa China nchini Senegal Li Zhigang.
Li alisema eneo la maonyesho la China lililoandaliwa na kampuni zaidi ya 20 za China, linaonyesha mafanikio na matarajio ya ushirikiano kati ya China na Senegal katika maeneo kama vile miundombinu, mawasiliano ya 5G, viwanda vya kisasa na teknolojia zenye kutoa kaboni chache.
Ameelezea matumaini yake kuwa jumuiya za wafanyabiashara wa nchi zote mbili zitajenga maelewano, kuoanisha mahitaji ya maendeleo na kujenga mustakabali wa pamoja.
Hadi sasa, kampuni zaidi ya 100 za China zimewekeza na kufanya shughuli zao nchini Senegal, zikijikita katika sekta mbalimbali zikiwemo za ujenzi wa miundombinu mikubwa kama vile barabara kuu, madaraja na bandari, vilevile utengenezaji wa chuma, kauri na vifaa vya ujenzi, pamoja na teknolojia ya kupashana habari na viwanda vya teknolojia ya hali ya juu.
Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi wa Jukwaa la Wekeza nchini Senegal 2025 mjini Diamniadio, Senegal, Oktoba 7, 2025. (Ikulu ya Rais wa Senegal/kupitia Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma