

Lugha Nyingine
Rais Xi kuhudhuria ufunguzi wa Mkutano wa Viongozi Duniani kuhusu Wanawake na kutoa hotuba kuu
BEIJING - Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Guo Jiakun ametangaza jana Alhamisi kwamba Mkutano wa Viongozi Duniani kuhusu Wanawake utafanyika Beijing, mji mkuu wa China kuanzia Oktoba 13 hadi 14 ambapo Rais wa China Xi Jinping atahudhuria kwenye ufunguzi wa mkutano huo na kutoa hotuba kuu.
Mkutano huo, ulioandaliwa kwa pamoja na China na Shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa (UN Women), utawakutanisha wakuu wa nchi, viongozi wa serikali, viongozi wa mabunge, manaibu mawaziri wakuu, maofisa wa wizara, viongozi wa mashirika ya kimataifa na watu marafiki kutoka mabara mbalimbali, msemaji Guo amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari.
Msemaji huyo amesema kuwa mwaka huu ni maadhimisho ya miaka 30 tangu kufanyika Mkutano wa Nne wa Wanawake wa Dunia mjini Beijing, ambao ulipitisha Azimio la Beijing na Mpango wa Utekelezaji, na amesema mkutano utakaofanyika utasisitiza tena moyo wa mkutano huo na kuharakisha utekelezaji wa matokeo yake.
Amesema mkutano huo utaleta msukumo mpya kwa ajili ya kuhimiza usawa wa jinsia na maendeleo ya wanawake kwa pande zote, na kuhimiza ujenzi wa jumuiya ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja.
Guo amesema China inatarajia kujiunga pamoja na jumuiya ya kimataifa katika kuhakikisha mkutano huo ujao unafanyika kwa mafanikio, ili kuufanya kuwa mnara mwingine katika historia ya maendeleo ya wanawake duniani.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma