

Lugha Nyingine
Kuandika ukurasa mpya wa Maendeleo ya Mambo ya Wanawake Duniani
Mkutano wa Viongozi Duniani kuhusu Wanawake utafanyika mjini Beijing kuanzia tarehe 13 hadi 14, Oktoba, ambapo rais Xi Jinping wa China atahudhuria kwenye ufunguzi wa mkutano huo na kutoa hotuba.
Mwaka huu ni maadhimisho ya miaka 30 tangu ulipofanyika Mkutano wa 4 wa Wanawake Duniani wa Beijing. Miaka 30 iliyopita, mkutano huo wa kimataifa ulipitisha Azimio la Beijing na Mpango wa Utekelezaji, ukiwa mnara wa maendeleo ya mambo ya wanawake duniani. Baada ya miaka 30, kutokana na pendekezo la rais Xi, China itafanya Mkutano wa Viongozi Duniani kuhusu Wanawake, ambao umevutia ufuatiliaji wa jumuiya ya kimataifa.
China ikiwa mwenyeji wa Mkutano wa 4 wa wanawake duniani wa Beijing, siku zote inafuata ahadi zake, ambapo inahimiza mambo ya wanawake kupata mafanikio ya kihistoria, huku ikitoa mchango muhimu kwa ajili ya mambo ya maendeleo ya wanawake duniani. Tokea zama mpya, rais Xi ametoa mfululizo wa mapendekezo na maoni muhimu kuhusu kuhimiza usawa wa jinsia na maendeleo ya wanawake wa pande zote. Mnamo mwaka 2015, rais Xi aliongoza Mkutano wa Viongozi Duniani kuhusu Wanawake uliofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York, ambapo alitoa mapendekezo manne muhimu yakiwemo “kuhimiza maendeleo ya wanawake yaende sambamba na maendeleo ya uchumi na jamii.” Mwaka 2020, katika mkutano wa ngazi ya juu wa kuadhimisha miaka 25 tangu kufanyika kwa mkutano wa 4 wa wanawake duniani wa Beijing wa Umoja wa Mataifa, rais Xi alitoa mapendekezo mengine muhimu, yakiwemo kuwasaidia wanawake kujitoa kutoka kwa athari ya uviko-19.
Kutoka kusukuma mbele ujenzi wa jumuiya ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja, hadi kuhimiza utekelezaji wa Pendekezo la Maendeleo ya Dunia, Pendekezo la Usalama wa Dunia, Pendekezo la Ustaarabu wa Dunia, na Pendekezo la Usimamizi wa Dunia, China imetoa mpango wa ufumbuzi wa kimfumo kwa ajili ya utekelezaji wa Azimio la Beijing na Mpango wa Utekelezaji.
Mambo ya wanawake ya China pia yamepata mafanikio makubwa. Wanawake milioni 690 nchini humu wamefikia wastani wa ustawi kwa pande zote, wanafunzi wa kike wanachukua nusu ya wanafunzi wanaosoma katika vyuo vikuu, na wafanyakazi wanawake wanachukua asilimia 45.8 ya wafanyakazi wote katika sekta za sayansi na teknolojia, n.k. Mafanikio ya mambo ya wanawake ya China yamepatikana kutokana na uhakikisho wa mifumo na uungaji mkono wa vitendo halisi. Kuhimiza usawa wa jinsia na maendeleo ya wanawake kwa pande zote kumewekwa kwenye mambo ya jumla ya maendeleo ya mambo ya ujamaa wenye umaalumu wa China, huku mfululizo wa sera zikilinda haki za wanawake.
China pia inafanya juhudi za kusaidia wanawake wa nchi nyingine nyingi kutimiza ndoto zao. China inashikilia ushirikiano wa pande nyingi, kuongoza na kuhimiza ajenda za maendeleo ya wanawake wa pande nyingi na wa kikanda. Kwa mfano, kuanzia mwaka 2012, China imefanya mikutano karibu 30 ya wanawake chini ya mifumo mingi ya ushirikiano, ikianzisha tuzo ya elimu ya watoto wa kike na wanawake pamoja na UNESCO. China imekusanya nguvu, kuchukua hatua za kivitendo zikiwemo "mradi wa afya ya wanawake na watoto" na "mpango wa chipukizi" na kuwawezesha wanawake wa nchi zinazoendelea kuboresha mazingira yao ya maisha na ya maendeleo. China imeimarisha mawasiliano kati ya watu, na kuchangia maarifa ya mafanikio yake katika maendeleo ya mambo ya wanawake, kama vile hadithi ya mwalimu Zhang Guimei inayosimuliwa sana kwenye jukwaa la UNESCO na mengine.
Hivi sasa mambo ya wanawake duniani bado yanakabiliwa na changamoto mbalimbali, kwa mfano, bado kuna wanawake na watoto wa kike zaidi ya milioni 600 wanaokumbwa na migongano na vurugu za vita, na wanawake na watoto wa kike bilioni 2 wanakosa uhakikisho wa kijamii. Katika kipindi kipya muhimu cha kihistoria, China ingependa kushirikiana na pande mbalimbali katika kusukuma mbele usawa wa jinsia na maendeleo ya wanawake kwa pande zote duniani, na kukusanya nguvu ya wanawake kwa ajili ya kujenga jumuiya ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja.
(Chanzo: People's Daily)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma