China yatetea udhibiti wa uuzaji nje wa madini adimu, yaitaka Marekani kushughulikia tofauti kupitia mazungumzo

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 13, 2025
China yatetea udhibiti wa uuzaji nje wa madini adimu, yaitaka Marekani kushughulikia tofauti kupitia mazungumzo
Picha iliyopigwa Agosti 19, 2025 ikionyesha meli ya mizigo kwenye Bandari ya Qingdao mjini Qingdao, Mkoani Shandong, mashariki mwa China. (Xinhua/Li Ziheng)

BEIJING - Wizara ya biashara ya China imetetea hatua za kudhibiti uuzaji nje wa madini adimu na bidhaa zinazohusiana ikizielezea kuwa ni hatua halali, huku ikiitaka Marekani kushughulikia ipasavyo tofauti kupitia mazungumzo na kwa msingi wa kuheshimiana na kujadiliana kwa usawa.

"China, ikiwa nchi kubwa inayowajibika, huchukua hatua za kudhibiti uuzaji nje bidhaa husika kwa mujibu wa sheria, ili kulinda vyema amani duniani na utulivu wa kikanda, na kutimiza wajibu wa kuzuia kuenea kwa silaha za nyuklia na wajibu mwingine wa kimataifa," msemaji wa wizara hiyo amesema jana Jumapili wakati akijibu maswali ya vyombo vya habari, akisema kuwa China imetilia maanani matumizi muhimu ya madini hayo adimu ya uzito wa kati na mkubwa na vitu vingine vinavyohusiana katika matumizi ya kijeshi.

Amesema, China imefanya tathmini ya kina kuhusu athari zitakazotokea za hatua hizo katika minyororo ya viwanda na usambazaji bidhaa mapema na ina uhakika kwamba athari husika ni ndogo sana, huku akisema kuwa kabla ya hatua hizo kutangazwa, China tayari ilikuwa imeziarifu nchi na maeneo husika kupitia utaratibu wa mazungumzo ya pande mbili ya udhibiti wa mauzo ya nje.

"Udhibiti huo wa China wa kuuza nje siyo marufuku ya kuuza nje. Maombi yote ya kuuza nje yanayokidhi masharti kwa matumizi ya kiraia yanaweza kupata kibali, ili kampuni husika zisiwe na haja ya kuwa na wasiwasi." amesema msemaji huyo.

Amesema, China inapenda kushirikiana na nchi nyingine duniani ili kuongeza mazungumzo na mawasiliano ya udhibiti wa mauzo ya nje, ili kulinda vyema usalama na utulivu wa minyororo ya viwanda na usambazaji bidhaa duniani.

"Kwenda mbele, serikali ya China itafanya mapitio kwa mujibu wa sheria na kanuni, kutoa leseni kwa maombi yanayostahiki, vilevile kuzingatia kikamilifu matumizi ya hatua wezeshi kama vile kutoa leseni za jumla na kusamehe leseni ili kuhimiza biashara halali," msemaji huyo amesema.

Akijibu swali kuhusu tangazo la Marekani la kuweka ushuru wa asilimia 100 kwa China na udhibiti wa mauzo ya nje kwa programu zote muhimu za kompyuta, msemaji huyo amesema China daima inachukua msimamo wa haki na wenye kanuni zenye mantiki na kutekeleza hatua za udhibiti wa mauzo ya nje kwa namna ya busara na ya wastani, wakati kauli za Marekani zinaonyesha namna ya "undumila kuwili."

"Kwa muda mrefu, Marekani imekuwa ikieneza dhana ya usalama wa taifa, kutumia vibaya udhibiti wa mauzo ya nje, kuchukua hatua za ubaguzi dhidi ya China, na kuweka hatua za upande mmoja za mamlaka ya mkono mrefu kwa bidhaa mbalimbali zikiwemo vifaa vya semiconductor na chipu," amesema msemaji huyo.

Msemaji huyo amesema, hatua hizo za Marekani zimeathiri vibaya haki na maslahi halali na ya kisheria ya kampuni, kuvuruga kwa kiasi kikubwa utaratibu wa kimataifa wa uchumi na biashara, na kuathiri sana usalama na utulivu wa minyororo ya viwanda na usambazaji bidhaa duniani.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha