

Lugha Nyingine
Waziri Mkuu wa China Li Qiang akutana na Rais wa Ghana John Dramani Mahama
Waziri Mkuu wa China Li Qiang akikutana na Rais John Dramani Mahama wa Ghana, ambaye yuko mjini Beijing kuhudhuria Mkutano wa Viongozi Duniani kuhusu Wanawake, kwenye Jumba la Wageni wa taifa la Diaoyutai mjini Beijing, mji mkuu wa China, Oktoba 13, 2025. (Xinhua/Huang Jingwen)
BEIJING - Waziri Mkuu wa China Li Qiang jana Jumatatu alikutana na Rais John Dramani Mahama wa Ghana, ambaye yuko Beijing kuhudhuria Mkutano wa Viongozi Duniani kuhusu Wanawake, akisema kuwa China na Ghana ziliinua uhusiano wa pande mbili kuwa ushirikiano wa kimkakati mwaka jana, zikiwa na fursa mpya za ushirikiano katika nyanja mbalimbali.
"China inapenda kushirikiana na Ghana kupanua ushirikiano wa kivitendo na kuongeza kwa kina ushirikiano wa kimkakati ili kuleta manufaa zaidi kwa watu wa nchi zote mbili," amesema.
Waziri Mkuu huyo amesisitiza kuwa China inapenda kusukuma mbele ushirikiano wa kiwango cha juu wa Ukanda Mmoja, Njia Moja na Ghana, kuzidisha ushirikiano katika biashara, uwekezaji, ujenzi wa miundombinu, kilimo, uvuvi na nishati, na kuhimiza mawasiliano katika elimu, utamaduni, utalii na afya.
“Zikiwa nchi kubwa za Nchi za Kusini, China na Ghana zinapaswa kufanya kazi pamoja ili kushikilia ushirikiano wa pande nyingi na biashara huria” Li ameongeza.
Kwa upande wake Rais Mahama ameipongeza China kwa kuandaa kwa mafanikio Mkutano wa Viongozi Duniani kuhusu Wanawake, akielezea shukrani za dhati kwa uungaji mkono wa muda mrefu wa China kwa Ghana, na kupongeza sera ya China ya kutoza ushuru-sifuri kwa nchi za Afrika ambazo zina uhusiano wa kidiplomasia na China.
Amesema Ghana inafuata kithabiti kanuni ya kuwepo kwa China moja, na inapenda kuzidisha ushirikiano na China katika biashara, uwekezaji, ujenzi wa miundombinu, nishati, kilimo na madini, wakati huohuo ikitafuta vichocheo vipya vya ukuaji katika maeneo kama vile uchumi wa kidijitali na akili mnemba.
Rais Mahama ameongeza kuwa Ghana inaunga mkono Pendekezo la Usimamizi wa Dunia, na itaendelea kushirikiana na China ili kushikilia kithabiti ushirikiano wa pande nyingi na kulinda haki na usawa wa kimataifa.
Waziri Mkuu wa China Li Qiang akikutana na Rais John Dramani Mahama wa Ghana, ambaye yuko mjini Beijing kuhudhuria Mkutano wa Viongozi Duniani kuhusu Wanawake, kwenye Jumba la Wageni wa Taifa la Diaoyutai mjini Beijing, mji mkuu wa China, Oktoba 13, 2025. (Xinhua/Huang Jingwen)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma