China yasema hatua zake za kudhibiti uuzaji nje wa madini adimu hazina uhusiano wowote na Pakistan

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 14, 2025

BEIJING - Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Lin Jian amesema hatua za hivi karibuni za nchi hiyo kudhibiti uuzaji nje wa madini adimu na bidhaa zinazohusiana nayo hazina uhusiano wowote na Pakistan, akisema kuwa hatua hizo ni utaratibu halali uliopitishwa na serikali ya China kuboresha mfumo wake wa udhibiti wa mauzo ya nje kwa mujibu wa sheria na kanuni.

Lin ameyasema hayo jana Jumatatu kwenye mkutano na wanahabari alipoulizwa kuzungumzia kuhusu vyombo vya habari vinasema Pakistan, kwa kutumia vifaa na teknolojia ya China, inauza nje madini adimu kwa Marekani, jambo ambalo linadaiwa kuwa limeifanya China kuanzisha kanuni hizo mpya kali za kudhibiti uuzaji nje wa teknolojia zinazohusiana na madini adimu.

Lin amesema kuwa China na Pakistan ni washirika wa kimkakati wa hali zote, na kwamba urafiki imara kama chuma kati ya nchi hizo mbili umeongezeka na kuwa imara zaidi baada ya muda uliopita.

Ameongeza kuwa pande hizo mbili daima zimekuwa zikidumisha hali ya kuaminiana kimkakati kwa ngazi ya juu na mawasiliano ya karibu katika masuala makuu yanayohusu maslahi ya pamoja ya pande zote mbili.

"Ninachofahamu, China na Pakistan zimezungumza kuhusu suala la ushirikiano wa madini kati ya Pakistan na Marekani. Pakistan imesisitiza kuwa mazungumzo yake na Marekani hayatadhuru kamwe maslahi ya China na ushirikiano kati ya China na Pakistan," amesema.

Amesema kuwa sampuli za madini zilizoonyeshwa na kuwasilishwa na viongozi wa Pakistani kwa wenzao wa Marekani ni sampuli za vito ghafi ambazo zilinunuliwa na mfanyakazi wao.

"Ripoti husika aidha zinatokana na ukosefu wa ufahamu wa uhalisia wa mambo, zina msingi wa uvumi, au zina nia ya kupanda mifarakano, na hazina mantiki kabisa" ameongeza.

Lin amesisitiza kuwa hatua hizo za udhibiti wa uuzaji nje zinalenga kulinda vyema amani ya dunia na utulivu wa kikanda, na kutimiza wajibu wa kimataifa kama vile ahadi za kutoeneza silaha.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha