

Lugha Nyingine
Mongella: Mkutano wa Beijing mwaka 1995 umebadilisha mawazo na namna ya kufikiri kuhusu maendeleo ya binadamu
Gertrude Mongella aliyekuwa Katibu Mkuu wa Mkutano wa Wanawake Duniani wa Beijing mwaka 1995 amesema miaka 30 tangu kufanyika mkutano huo kuna matokeo makubwa yamepatikana ambayo yamebadilisha mawazo na namna ya kufikiri kuhusu maendeleo ya binadamu, akipongeza hotuba kuu ya Rais Xi Jinping wa China aliyoitoa jana Jumatatu kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Viongozi Duniani kuhusu Wanawake mjini Beijing akisema imeweka msukumo mpya katika kuharakisha mchakato wa maendeleo ya wanawake.
Amesema, mkutano huo ambao ulikuwa wa nne tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa, katika maazimio yake ulitambua umuhimu wa kuona kwamba binadamu wote awe mwanamke au mwanaume ni sawa na kwamba haki za wanawake ni sawa na haki nyingine za binadamu.
"Kwa hiyo huu mkutano ulikuwa muhimu katika kubadilisha mawazo yaliyokuwepo huko zamani ambapo wanawake duniani kote walionekana ni watu hawana umuhimu kama walivyo wanaume" amesema Mongella, ambaye watu wengi pia humwita "mama Beijing" kutokana na mchango wake katika mkutano huo.
Amefafanua kuwa, kabla ya mkutano huo dunia ilikuwa ikijinyima fursa ya wanawume na wanawake kufanya kazi kwa pamoja huku nusu tu ya binadamu kwa maana ya wanaume wakiwa ndiyo wanaonekana wa maana wakati nusu nyingine ya wanawake ikiachwa nyuma.
“Kwa hiyo sasa tumefika mahali ambapo dunia inaona ya kwamba ni muhimu kuondoa vizuizi vyote na tuweze kuhakikisha ya kwamba tunaondoka kwa pamoja” ameongeza.
Aidha, amesema mafanikio mengine ni ajenda hiyo ya wanawake kwa sasa kuwa ajenda muhimu sana tofauti na zamani ambapo mtu akizungumza masuala ya wanawake alionekana kwa kila mmoja kuwa aliyepitwa na wakati kwa kuzungumza mambo ya wanawake ambayo hayakuwa na maana.
"Lakini sasa hivi wanawake ni ajenda muhimu katika jamii" amesisitiza.
Amesema jamii sasa imeweza kuona umuhimu wa kuangalia maendeleo ya wanawake ili kuharikisha maendeleo ya taifa. Amesema hilo linaifanya dunia ione kwamba mkutano wa Beijing na maudhui yake umekuwa wa muhimu sana duniani.
"Sasa hivi, katika nchi nyingi kumnyanyasa mwanamke, hatua za kisheria zinaweza kuchukuliwa. Sheria zimebadilika ili kumlinda mwanamke, ili kumlinda mtoto wa kike... kwa mfano sasa hivi mwanamke akibakwa na mtu akapatikana na kosa anaweza kufungwa miaka 30 jela kwa Tanzania. Na nchi nyingi zimefanya hivyo kuzuia ukatili wa kijinsia" ameongeza.
Ametaja mafanikio mengine mbalimbali katika harakati ya wanawake kuwa ni pamoja na wanawake sasa kuweza kupata ajira zaidi kuliko miaka ya nyuma, wanapewa nafasi katika ngazi za uongozi kuliko zamani ambapo walikuwa wakifanya kazi za chini, lakini pia kutokana na elimu zao wanaweza kuajiriwa katika ngazi za juu za maamuzi.
Akizungumzia mafanikio ya China katika masuala ya wanawake, Mongella ambaye pia alikuwa mjumbe wa Kundi la Washauri wa Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Kwa ajili ya Kufuatilia Utekelezaji wa Azimio la Beijing Barani Afrika Kusini mwa Sahara, amesema China imejitahidi sana kuleta mabadiliko.
Amesema, katika azimio la Beijing, suala la umaskini lilikuwa moja ya masuala muhimu yaliyotiliwa mkazo kwamba wanawake wanakandamizwa na umaskini uliokithiri wakishindwa kuingia katika mambo mengine ya maendeleo kwa sababu ya hali ya umaskini.
"China imebadilisha hali hiyo kabisa...wanawake wengi wameinuliwa katika dimbwi la umaskini na sasa hivi wako katika uchumi wa kati, kwa hiyo hilo ni mojawapo. Lakini pia ajira kwa wanawake imeongezeka katika nchi ya China na pia ujuzi wa akina mama katika nyanja mbalimbali afya, elimu na uongozi umeongezeka” amesema
Mongella amepongeza hotuba kuu ya Rais wa China aliyoitoa kwenye ufunguzi wa mkutano huo wa mwaka huu wa wanawake, akisema kuwa imetoa msukumo na mapendekezo ya namna ya kwenda mbele kuhakikisha maendeleo ya wanawake.
"Imetoa mapendekezo ya hatua tunazoweza tukafanya na ambazo zimeandaliwa kufanyika China ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa maazimio tuliyo azimia miaka 30 nyuma" amesema.
Kuhusu fursa ya China kushirikiana na nchi nyingine zinazoendelea katika kusukuma mbele ajenda ya wanawake na usawa wa kijinsia, Mongella amesema, kuna haja ya kushirikiana zaidi katika kubadilishana mawazo, teknolojia na kufanya mapinduzi ya maendeleo kwa pamoja. Ameongeza kuwa, China imepiga hatua kubwa katika maendeleo ya kidijitali hivyo kuna haja ya kushirikiana pia katika nyanja hiyo.
Mongella pia ametoa ushauri kwa wanawake duniani katika kuendeleza harakati zao akisema kuwa wanapaswa kuacha kusubiri kufanyiwa na wengine bali wawe na utayari, jitihada na kuonesha uwezo wao wenyewe katika kujiletea maendeleo na kujiondoa katika umaskini. Amesisitiza haja ya kuwa na ari ya kujiendeleza kielimu na kutafuta maarifa mapya kila wakati huku serikali zikiwezesha.
Mkutano wa Viongozi Duniani kuhusu Wanawake, ulioandaliwa kwa pamoja na China na Shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa (UN Women) umefanyika Beijing, mji mkuu wa China kwa siku mbili za jana Jumatatu Oktoba 13 na leo Jumanne, Oktoba 14. Mongella yuko Beijing, China, kuhudhuria mkutano huo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma