

Lugha Nyingine
Rais Xi Jinping akutana na Rais wa Ghana John Dramani Mahama
Rais Xi Jinping wa China akikutana na Rais John Dramani Mahama wa Ghana, ambaye yuko Beijing kuhudhuria Mkutano wa Viongozi Duniani kuhusu Wanawake, kwenye Jumba la Mikutano ya Umma la Beijing, mji mkuu wa China, Oktoba 14, 2025. (Xinhua/Xie Huanchi)
BEIJING - Rais Xi Jinping wa China amekutana na Rais John Dramani Mahama wa Ghana jana Jumanne, ambaye yuko mjini Beijing kuhudhuria Mkutano wa Viongozi Duniani kuhusu Wanawake, akisema kuwa mwaka huu ni maadhimisho ya miaka 65 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Ghana, na China inapenda kushirikiana na Ghana kuhimiza uboreshaji wa ushirikiano katika sekta mbalimbali na kutoa mchango mkubwa zaidi katika kujenga jumuiya ya China na Afrika yenye mustakabali wa pamoja katika zama mpya.
Amesema kuwa China inapenda kuongeza hali ya kuaminiana kisiasa na Ghana na kuungana mkono katika masuala yanayohusu maslahi yao ya msingi na mambo yanayofuatiliwa na kila mmoja wao.
Rais Xi ametoa wito kwa pande hizo mbili kutekeleza kwa pamoja matokeo ya mkutano wa kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) wa Beijing mwaka 2024, kutafuta miundo ya ushirikiano wa aina mbalimbali, kupanua ushirikiano katika sekta mbalimbali, zikiwemo madini, nishati, ujenzi wa miundombinu, kilimo na uvuvi, na kuisaidia Ghana kugeuza faida zake bora za rasilimali kuwa msukumo wa maendeleo.
Rais Xi ameeleza matumaini yake kuwa Ghana itafaidika kutoka kwenye utozaji ushuru-sifuri wa China kwa asilimia 100 ya bidhaa zinazostahiki kutozwa ushuru wa forodha kwa nchi za Afrika ambazo zina uhusiano wa kidiplomasia nayo katika siku za karibuni.
Kwa upande wake Rais Mahama ameipongeza China kwa kuandaa kwa mafanikio Mkutano wa Viongozi Duniani kuhusu Wanawake, akisema kwamba ulikuwa na umuhimu mkubwa na umedhihirisha uongozi wa China katika kusukuma mbele maendeleo ya wanawake duniani.
Amesema Ghana inafuata bila kuyumba sera ya kuwepo kwa China moja na imedhamiria kuimarisha uhusiano wake na China. Ameeleza matumaini yake kuwa Ghana itaimarisha ushirikiano na China katika biashara, uchumi wa kidijitali, ujenzi wa miundombinu, nishati, madini na mawasiliano ya kitamaduni na ya kati ya watu.
Rais Mahama ameongeza kuwa Ghana inashikilia kithabiti mfumo wa pande nyingi, inatekeleza Pendekezo la Usimamizi Duniani, na imedhamiria kulinda haki na usawa wa kimataifa.
Rais Xi Jinping wa China akikutana na Rais John Dramani Mahama wa Ghana, ambaye yuko Beijing kuhudhuria Mkutano wa Viongozi Duniani kuhusu Wanawake, kwenye Jumba la Mikutano ya Umma mjini Beijing, mji mkuu wa China, Oktoba 14, 2025. (Xinhua/Zhai Jianlan)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma