China yasema udhibiti wake wa uuzaji nje wa madini adimu unaendana na desturi ya kimataifa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 16, 2025

BEIJING - China imechukua hatua za udhibiti wa uuzaji nje madini adimu na vitu vinavyohusika kwa mujibu wa sheria, ambayo inaendana na desturi ya kimataifa, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Lin Jian amesema jana Jumatano wakati akijibu kauli za Mwakilishi wa Biashara wa Marekani Jamieson Greer, ambaye alisema kwamba kama ushuru wa ziada wa asilimia 100 kwa bidhaa za China utaanza kutekelezwa Novemba 1 au mapema zaidi, itategemea na kile China itakachofanya.

Greer pia alisema maafisa wa China wametoa kauli zinazokinzana kuhusu vizuizi hivyo vya hivi karibuni vya uuzaji nje madini adimu.

Lin amesema mamlaka husika zimeweka wazi msimamo wa China kuhusu hatua hizo za udhibiti wa uuzaji nje madini adimu na vitu vingine vinavyohusika, akiongeza kuwa China imechukua hatua za kulinda vyema amani ya dunia na utulivu wa kikanda, na kutimiza wajibu wa kutoeneza silaha na wajibu mwingine wa kimataifa.

"Msimamo wa China umekuwa thabiti na wazi," msemaji huyo amesema, akiongeza kuwa ni Marekani ambayo inaomba mazungumzo huku ikitishia ushuru wa juu na vizuizi vipya, ambayo si njia sahihi kwa China.

Lin amesema China inaitaka Marekani isahihishe mbinu yake potovu mapema iwezekanavyo na kushughulikia masuala husika kupitia mazungumzo na majadiliano juu ya msingi wa usawa, kuheshimiana na kunufaishana.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha