Jeshi la Madagascar latangaza kuchukua mamlaka ya serikali

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 16, 2025

Kanali Michael Randrianirina (katikati), afisa wa kijeshi wa Madagascar, akihudhuria mkutano kati ya maafisa wa kijeshi na wabunge, mjini Antananarivo, Madagascar, Oktoba 14, 2025. (Picha na Sitraka Rajaonarison/Xinhua)

Kanali Michael Randrianirina (katikati), afisa wa kijeshi wa Madagascar, akionekana katika ikulu ya rais mjini Antananarivo, Madagascar, Oktoba 14, 2025. (Picha/cfp)

ANTANANARIVO - Kanali Michael Randrianirina, afisa wa kijeshi wa Madagascar, ametangaza Jumanne wiki hii kwamba mamlaka ya serikali nchini Madagascar yamechukuliwa rasmi na baraza la kijeshi linalojumuisha askari wa jeshi, gendarmerie na polisi wa kitaifa.

"Tuko hapa kuchukua madaraka," amesema Randrianirina, akiongeza kuwa uamuzi huo umefuata "wamegundua kuwa na hali ya kutofuata Katiba na kukiukwa kwa haki za binadamu."

Randrianirina amesema katiba imesimamishwa na miundo mipya ya kitaifa imeanzishwa "kukidhi matakwa ya watu wa Madagascar." Pia ametangaza kuvunjwa kwa taasisi muhimu za umma, zikiwemo Seneti, Mahakama Kuu ya Kikatiba na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

"Katika siku zijazo, serikali ya kiraia itaundwa," amesema, akiongeza kuwa dhamira yake itakuwa kuongoza ustawi wa taifa, kurejesha imani ya umma kwa taasisi, na kujenga upya serikali inayotilia maanani haki, utawala bora na uwajibikaji.

Akisisitiza kwamba muhula wa muundo huo wa mpito umewekwa katika kikomo cha muda wa juu wa miaka miwili, amesema kuwa kura ya maoni inayofuata katiba itaandaliwa, ikifuatiwa na uchaguzi mkuu ili kuanzisha taasisi mpya.

Siku hiyo hiyo, Bunge la Madagascar, baraza la chini la nchi hiyo yenye mabunge mawili, lilipiga kura ya kumwondoa madarakani Rais Andry Rajoelina wakati wa kikao maalum katika mji mkuu, Antananarivo, licha ya tangazo la awali la Ikulu ya Rais kwamba bunge hilo limevunjwa.

"Kuondolewa madarakani kwa Rais Andry Rajoelina kumepigiwa kura. Miongoni mwa wabunge 131 waliokuwepo wakati wa kupiga kura, 130 wamepiga kura ya ndio, huku mmoja amejizuia kupiga kura," amesema Naibu Spika wa bunge hilo Siteny Randrianasoloniaiko, kufuatia kikao hicho.

Uamuzi huo umekuja saa chache baada ya Rajoelina kutangaza kulivunja Bunge hilo.

Vyombo vya habari nchini humo vimemnukuu Randrianasoloniaiko akisema kuwa amri ya kuvunjwa "haikuwa na uhalali wa kisheria kutokana na kutokuwepo kwa uthibitisho rasmi."

Maandamano yalizuka nchini Madagascar mwishoni mwa Septemba, ambayo hapo awali yalichochewa na kukatika kwa umeme na ukosefu wa maji. Baadhi ya maandamano yaligeuka kuwa ya vurugu na hivi karibuni yalizidi hadi kuwa wito wa kutaka rais ajiuzulu.

Maandamano hayo yalichukua sura mpya mpya siku ya Jumamosi, huku kikosi cha jeshi kikitangaza kuyaunga mkono na kulinda waandamanaji.

Katika taarifa yake siku ya Jumapili, Ofisi ya Rais wa Madagascar ilisema kuwa "jaribio la kuchukua mamlaka kinyume cha sheria na kwa nguvu" linaendelea nchini Madagascar. Ilitoa wito kwa vikosi vyote muhimu vya taifa "kuungana pamoja ili kulinda utaratibu wa kikatiba na mamlaka ya kitaifa."

Siku ya Jumatatu, Rajoelina alisema katika video iliyochapishwa kwenye mtandao wa kijamii kwamba alikuwa amekimbilia "mahali salama." Alidai kuwa alikuwa mlengwa wa jaribio la mauaji lililoratibiwa na "wanajeshi waliochochewa na wanasiasa."

Hakueleza mahali hasa alipokuwa lakini alisema kuwa njia pekee ya kutoka kwenye msukosuko huo ni kupitia kuheshimu katiba.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha