Rais wa Tanzania atangaza Baraza jipya la mawaziri

(CRI Online) Novemba 18, 2025

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametangaza Baraza jipya la mawaziri jana Jumatatu lenye wajumbe 27, akibakiza baadhi ya mawaziri muhimu wakati huohuo akiteua wengine wapya katika wizara za kimkakati.

Katika hotuba yake aliyotoa kupitia matangazo ya moja kwa moja ya televisheni kutoka Ikulu ya Chamwino mjini Dodoma, Rais Samia amethibitisha kuwa Mahmoud Thabit Kombo ataendelea kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Khamis Mussa Omar ameteuliwa kuwa Waziri mpya wa fedha, akichukua nafasi ya Mwigulu Nchemba ambaye hivi karibuni aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu.

Rais huyo pia amemteua Rhimo Simeon Nyansaho kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, akichukua nafasi ya Stergomena Lawrence ambaye amestaafu utumishi wa umma.

Kama sehemu ya mabadiliko muundo wa baraza hilo, Rais Samia ametangaza kuundwa kwa Wizara mpya itakayojikita katika maendeleo ya vijana, akisisitiza umakini wa serikali katika kuwezesha vijana.

Mawaziri hao wateule wanatarajiwa kuapishwa leo Jumanne katika Ikulu ya Chamwino.

(Wahariri wa tovuti:Liu Mengxue,Renato Lu)

Picha