Lugha Nyingine
Kongamano lafanyika mjini Cape Town, Afrika Kusini kuadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa FOCAC
Picha hii iliyopigwa Oktoba 20, 2025, ikionyesha mandhari ya Ufukwe wa V&A mjini Cape Town, Afrika Kusini. (Xinhua/Han Xu)
CAPE TOWN - Taasisi ya Utafiti ya Jamii Jumuishi ya Afrika Kusini (ISI) na Chuo Kikuu cha Ualimu cha Zhejiang cha China zilifanya kongamano mjini Cape Town, Afrika Kusini Jumatatu wiki hii kuadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC).
Wawakilishi kutoka ISI na Taasisi ya Masomo kuhusu Afrika katika Chuo Kikuu cha Ualimu cha Zhejiang walifanya majadiliano ya kina kwenye Kituo cha Kwanza cha Urithi wa Mataifa katika mji mkuu huo wa bunge, Cape Town.
Kwenye hotuba yake kuu, Mkurugenzi Mtendaji wa ISI Daryl Swanepoel amesema FOCAC imekuwa "nguzo muhimu ya ushirikiano wa Kusini na Kusini katika zama mpya."
"Kwa Afrika, FOCAC inatoa jukwaa la kuongeza ushiriki katika kuunda ushirikiano wake wa maendeleo, na kwa China, inaashiria mbinu iliyokomaa kwa maendeleo duniani ambayo imejengwa katika msingi wa uendelevu, ushirikiano, na kujifunza kwa pamoja," amesema.
Liu Hongwu, mkurugenzi wa Taasisi ya Masomo kuhusu Afrika, amesisitiza umuhimu wa Afrika Kusini katika ushirikiano kati ya China na Afrika na ushirikiano pana wa Kusini na Kusini.
"Tumekuja hapa kuendeleza ushirikiano huo. Si tu tunafanya kazi pamoja chini ya FOCAC, lakini pia tunadumisha mawasiliano ya ngazi ya juu kati ya watu wa China na Afrika Kusini," Liu amesema.
Ameongeza kuwa mazungumzo na mawasiliano hayo ya ana kwa ana yanawezesha pande zote mbili kuelewana vyema leo na katika siku za baadaye, ikikuza jamii jumuishi zaidi iliyojengwa juu ya umoja.
Watu wakipiga picha na Mlima Meza mjini Cape Town, Afrika Kusini, Oktoba 20, 2025. (Xinhua/Han Xu)
Wang Xiao, kaimu konsuli mkuu wa Ubalozi wa China mjini Cape Town, amesisitiza kuwa katika miaka 25 iliyopita, FOCAC imekua na kuwa jukwaa pana linalojumuisha mazungumzo ya kisiasa, biashara na uwekezaji, miundombinu, elimu, utamaduni, afya ya umma, na amani na usalama.
"Imeleta manufaa halisi kwa watu wa China na Afrika na kuwa ishara yenye nguvu ya ushirikiano wa Kusini na Kusini. Ushirikiano wetu umekuwa ukiongozwa kwa kuheshimiana, usawa, na dhamira thabiti kwa maendeleo ya kila mmoja." Wang amesema.
Amesema ushirikiano huo haulazimishwi kwa nguvu za nje, wala kuundwa kwa ushindani wa kiitikadi; na kwamba umetokana na urafiki wa kweli, matarajio ya pamoja, na maslahi ya pamoja.
Picha hii iliyopigwa Oktoba 20, 2025, ikionyesha mandhari ya mtaani kwenye eneo la ufukwe wa V&A mjini Cape Town, Afrika Kusini. (Xinhua/Han Xu)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



