Lugha Nyingine
Erdogan na Zelensky wafanya mazungumzo mjini Ankara kwa ajili ya kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na Russia
ANKARA - Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesisitiza dhamira ya Uturuki katika kusukuma mbele juhudi za kidiplomasia za kumaliza mgogoro kati ya Russia na Ukraine, kwenye mazungumzo na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine mjini Ankara jana Jumatano.
"Itakuwa vyema kwa mchakato wa Istanbul kuanzishwa tena kwa mfumokazi wa pande zote ambao unaweza kukabiliana na matatizo makubwa ya sasa," Rais Erdogan amesema kwenye mkutano wao wa pamoja na waandishi wa habari, akitoa wito wa uungaji mkono mpya wa kimataifa kwa mpango huo.
Amesisitiza kwamba Uturuki inapenda kujadili na Russia "mapendekezo yoyote ambayo yanaweza kuharakisha kusimamisha mapigano na kuandaa njia kwa ajili ya amani ya haki na ya kudumu," huku akiwahimiza washirika wote wanaotafuta kusimamisha umwagaji damu huo kutumia mbinu ya kiujenzi kuanzisha tena mchakato huo.
Russia na Ukraine zilifanya duru ya tatu ya mazungumzo ya amani mjini Istanbul Julai 23, 2025, zikikubaliana kubadilishana wafungwa lakini hazikupiga hatua yoyote kuelekea kumaliza mgogoro huo unaoendelea.
Kwa upande wake Rais Zelensky, amesema Ukraine inatarajia kuanzisha tena kubadilishana wafungwa ifikapo mwisho wa mwaka huu.
"Uturuki inatoa uungaji mkono mkubwa katika suala hili," amesema, akiongeza kuwa Kiev inaamini "nguvu ya diplomasia ya Uturuki na uwezo wake wa kueleweka na Russia."
Amemshukuru Rais Erdogan kwa msimamo wa Uturuki katika kipindi chote cha mgogoro huo.
"Msimamo wa Uturuki juu ya vita na Russia ni muhimu sana kwa Ukraine," amesema kiongozi huyo wa Ukraine, akieleza shukrani kwa "ushirikiano na Uturuki unaosaidia kulinda maisha, na mtazamo dhahiri wa Uturuki kwa mambo yote muhimu" ya mgogoro huo unaoendelea nchini Ukraine.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



