Lugha Nyingine
China yatangaza uungaji mkono wa kinga na tiba ya VVU wenye thamani ya dola milioni 3.49 kwa Afrika Kusini

Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS Winnie Byanyima akitotoa hotuba kwenye hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Kuzuia VVU mjini Johannesburg, Afrika Kusini, Novemba 20, 2025. (Xinhua/Chen Wei)
JOHANNESBURG - Ili kukabiliana na VVU/UKIMWI nchini Afrika Kusini, kwa kupitia Mfuko wa China wa Maendeleo ya Dunia na Ushirikiano wa Kusini-Kusini, China imetangaza ahadi ya ufadhili wa miaka miwili wenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 3.49 ambapo makubaliano hayo, yaliyoratibiwa na UNAIDS, yametangazwa rasmi jana Alhamisi katika hafla iliyofanyika kwenye Ubalozi wa China mjini Pretoria, Afrika Kusini.
Afrika Kusini, ambayo ina watu takriban milioni 8 wanaoishi na VVU na milioni karibu 6 wanaotumia matibabu ya kupunguza makali ya virusi vya UKIWMI, ambapo imekuwa ikifanya juhudi za kupunguza maambukizi mapya, hasa miongoni mwa watu wa makundi muhimu ya vijana wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 24 ambao wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa VVU.
Uwekezaji huo katika mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI umekaribishwa katika hali ya kupunguzwa kwa fedha husika.
Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS Winnie Byanyima amesema uwekezaji huo unaonyesha ahadi ya China kwa ushirikiano wa pande nyingi na ushirikiano kati ya nchi za kusini za Dunia.
"Inaonyesha ahadi ya China kwa ushirikiano wa pande nyingi na kusukuma mbele ushirikiano kati ya Kusini-Kusini, kupitia kuchangia teknolojia, uvumbuzi, na ufadhili kwa kunufaishana pamoja ili kutimiza malengo ya kupata huduma ya afya kwa wote na lengo la kukomesha UKIMWI ifikapo mwaka 2030," amesema.
Mradi huo wa miaka miwili, wenye thamani ya mamilioni ya dola unatarajiwa kuwanufaisha vijana na vijana wazima 54,000 , hasa wale wanafunzi walio katika vyuo vya kazi za ufundi katika majimbo saba.
Balozi wa China nchini Afrika Kusini Wu Peng amesema mradi huo ni hatua madhubuti katika kutekeleza Pendekezo la Maendeleo ya Dunia na kujenga kwa pamoja jumuiya ya kimataifa ya afya kwa wote.
"China inaunga mkono kithabiti Afrika Kusini kuimarisha mradi wake wa kuzuia na kutibu VVU. Mbali na mradi huu, tuko tayari kuisaidia Afrika Kusini katika kuanzisha mfumo endelevu wa kukabiliana na VVU/UKIMWI kwa kupitia mazungumzo ya sera, utoaji wa dawa za kivumbuzi, uhamishaji wa teknolojia, na ujengaji wa uwezo. Tutaendelea kufanya juhudi za pamoja ili kujenga mustakabali mzuri zaidi na wa himilivu zaidi kwa nchi zetu mbili " amesema.
Baada ya hafla hiyo, Waziri wa Afya wa Afrika Kusini Aaron Motsoaledi ameeleza kukaribisha mpango huo, akisema mradi huo utaunga mkono juhudi za kupunguza maambukizi miongoni mwa vijana.
"Kila mchango ni muhimu katika mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI. Kupambana na ugonjwa huu kunahitaji hatua za pamoja kutoka kwa kila mmoja," amesema.

Balozi wa China nchini Afrika Kusini Wu Peng akitoa hotuba kwenye hafla ya Uzinduzi wa Mradi wa Kuzuia VVU mjini Johannesburg, Afrika Kusini, Novemba 20, 2025. (Xinhua/Chen Wei)

Waziri wa Afya wa Afrika ya Kusini Aaron Motsoaledi akitoa hotuba kwenye hafla ya Uzinduzi wa Mradi wa Kuzuia VVU mjini Johannesburg, Afrika Kusini, Novemba 20, 2025. (Xinhua/Chen Wei)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



