Lugha Nyingine
Waziri Mkuu wa China aihimiza G20 kujitahidi kwa ushirikiano mpana zaidi duniani kwa ajili ya maendeleo

Waziri Mkuu wa China Li Qiang akihutubia kikao cha tatu cha Mkutano wa 20 wa Kundi la 20 (G20) mjini Johannesburg, Afrika Kusini, Novemba 23, 2025. (Xinhua/Huang Jingwen)
JOHANNESBURG - Waziri Mkuu wa China Li Qiang ametoa wito wa juhudi za Kundi la nchi 20 (G20) kujitahidi kwa ushirikiano mpana zaidi duniani ili kukabiliana na changamoto kwa pamoja na kuhimiza maendeleo kwenye hotuba yake wakati akihudhuria kikao cha pili na cha tatu cha Mkutano wa 20 wa Viongozi wa G20 uliofanyika kwa siku mbili za Jumamosi na Jumapili mjini Johannesburg, Afrika Kusini.
"Kwa kuwa changamoto mbalimbali kama vile mabadiliko ya tabianchi, nishati na misukosuko ya chakula zinaingiliana, jumuiya ya kimataifa inahitaji kuungana ili kuweka nguvu pamoja na kutatua matatizo kupitia ushirikiano," Li amesema.
Kwanza, Waziri Mkuu Li ametoa wito kwa pande zote kuimarisha ushirikiano wa ikolojia na ulinzi wa mazingira, na kuongeza uhimilivu wa maendeleo. Ametoa wito kwa nchi na pande za G20 kuheshimu moyo wa kisayansi na kushikilia kanuni ya wajibu wa pamoja lakini wenye tofauti katika kukabiliana na masuala yanayohusu mabadiliko ya tabianchi na ikolojia.
"Kuhusu ushirikiano katika maeneo kama haya, pande zote zinapaswa kuonyesha uwajibikaji na kuchukua hatua kwa wakati," amesema.
Pili, Waziri Mkuu Li amehimiza juhudi za kuimarisha ushirikiano katika nishati ya kijani na kusukuma mbele mpito kuelekea nishati za kijani ulio wa haki.
Ametoa wito wa kuhimiza ushirikiano duniani katika sekta ya kijani, kuiweka minyororo ya viwanda na usambazaji bidhaa katika hali tulivu na isiyo na vizuizi, na kuwezesha mtiririko huru na matumizi ya teknolojia na bidhaa husika.
Tatu, amesema ushirikiano katika usalama wa chakula unapaswa kuimarishwa ili kuhakikisha usambazaji tulivu.
Waziri Mkuu Li ametoa wito wa kuboresha mzunguko na usambazaji wa chakula duniani, kujenga ushirikiano katika bidhaa muhimu, kuunda soko la chakula duniani lililo wazi, tulivu na endelevu, na kuimarisha usambazaji kwa ajili ya nchi zinazokabiliwa na uhaba wa chakula.
Wakati huo huo, waziri mkuu huyo wa China ametoa wito kwa nchi za G20 kuimarisha ushirikiano katika sayansi na teknolojia ya kilimo, ili kuongeza uwezo wa uzalishaji wa chakula.
"Duru mpya ya mapinduzi ya kisayansi na kiteknolojia na mageuzi ya viwanda inaharakishwa, ikileta fursa za maendeleo ambazo hazijawahi kutokea duniani, lakini pia inaweza kujenga hali mpya za ukosefu wa usawa na mapengo ya maendeleo," Li amesema.
Ameongeza kuwa G20 inapaswa kuhimiza pande zote kutilia maanani ufunguaji mlango, ushirikiano wa kunufaishana na fursa za pamoja, na kujitahidi kuboresha ustawi wa watu duniani kote.
Wakati wa mkutano huo, Waziri Mkuu Li alifanya mazungumzo ya kirafiki na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Rais wa Korea Kusini Lee Jae-myung, Rais wa Angola Joao Lourenco, Waziri Mkuu wa Hispania Pedro Sanchez, Mkurugenzi Mkuu wa WTO Ngozi Okonjo-Iweala, na wengine.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



