Lugha Nyingine
Waziri mkuu wa China asema, China inaahidi kuzidisha ushirikiano na Afrika Kusini

Waziri Mkuu wa China Li Qiang akikutana na Naibu Rais wa Afrika Kusini Paul Mashatile mjini Johannesburg, Afrika Kusini, Novemba 23, 2025. (Xinhua/Shen Hong)
JOHANNESBURG - China inapenda kushirikiana na Afrika Kusini ili kuimarisha kuungana mkono bila kuyumbayumba na kuzidisha ushirikiano wa kunufaishana, Waziri Mkuu wa China Li Qiang amesema jana Jumapili alipokutana na Naibu Rais wa Afrika Kusini Paul Mashatile pembezoni mwa Mkutano wa 20 wa Viongozi wa Kundi la 20 (G20) uliofanyika mjini Johannesburg, Afrika Kusini Jumamosi na Jumapili.
"China na Afrika Kusini ni marafiki na ndugu zikiwa na urafiki wa kina," Waziri Mkuu Li amesema, akiongeza kuwa mwezi Septemba mwaka jana, Rais Xi Jinping wa China alikutana na mwenzake wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, mjini Beijing na kufikia makubaliano muhimu kuhusu kusukuma mbele uhusiano wa pande mbili.
"China inapenda kushirikiana na Afrika Kusini kutekeleza mwongozo wa kimkakati wa wakuu hao wawili, kuongeza zaidi hali ya kuaminiana kisiasa, kuungana mkono bila kuyumbayumba, kuzidisha ushirikiano wa kunufaishana, ili kupata matokeo mapya zaidi ya ushirikiano wao wa kimkakati wa pande zote katika zama mpya" amesema.
Waziri Mkuu Li amesema kuwa China inapenda kuimarisha uratibu na Afrika Kusini, na kusaidia bidhaa zaidi za Afrika Kusini zenye ubora na ushindani kuingia katika soko la China kupitia mazungumzo na kusaini makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi kwa ajili ya maendeleo ya pamoja, na kusukuma mbele utekelezaji wa sera ya China kutotoza ushuru kwa asilimia 100 ya bidhaa kutoka nchi za Afrika zenye uhusiano wa kidiplomasia na China, na kuhimiza utekelezaji wake mapema nchini Afrika Kusini.
"China inaunga mkono kampuni za China zenye ushindani zaidi kuwekeza Afrika Kusini na kuimarisha ushirikiano katika maeneo kama vile nishati mpya, magari, huduma za afya, uchumi wa kidijitali na miundombinu, kwa lengo la kupanua na kupandisha hadhi ushirikiano wa pande mbili ili kupanua fursa za ushirikiano katika mchakato wa ujenzi wa mambo ya kisasa wa nchi zote mbili," amesema.
Ameelezea matumaini kwamba Afrika Kusini itaendelea kulinda vyema haki na maslahi halali ya kampuni za China na usalama wa wafanyakazi wao.
Waziri Mkuu Li ametoa wito kwa pande hizo mbili kuongeza uratibu wa pande nyingi na kushirikiana na nchi nyingi zaidi za Kusini ili kuhimiza utaratibu wa kimataifa ulio wa haki na usawa zaidi.
Kwa upande wake, Mashatile ametoa shukrani kwa uungaji mkono mkubwa wa China kwa Afrika Kusini kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Viongozi wa G20.
Huku akisisitiza kwamba Afrika Kusini inashikilia kithabiti sera ya kuwepo kwa China moja, Mashatile amesema kwamba nchi yake inapenda kuchukua sera ya China wa kutotoza ushuru kwa bidhaa kutoka nchi za Afrika kama fursa ya kuimarisha ushirikiano wa pande mbili katika uchumi na biashara, viwanda, kilimo, uchumi wa kidijitali na maendeleo ya kijani, na kuboresha mawasiliano ya watu ili kuendeleza zaidi ushirikiano wa kina na wa kimkakati wa pande zote katika zama mpya kati ya nchi hizo mbili.

Waziri Mkuu wa China Li Qiang akikutana na Naibu Rais wa Afrika Kusini Paul Mashatile mjini Johannesburg, Afrika Kusini, Novemba 23, 2025. (Xinhua/Zhai Jianlan)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



