Lugha Nyingine
Mkutano wa Viongozi wa G20 wa Johannesburg wapitisha taarifa ya pamoja licha ya Marekani kususia

Watu wakitembea kuipita nembo ya Mkutano wa 20 wa Viongozi wa Kundi la 20 (G20) mjini Johannesburg, Afrika Kusini, Novemba 22, 2025. (Xinhua/Chen Wei)
JOHANNESBURG - Mkutano wa 20 wa Viongozi wa Kundi la Nchi 20 (G20) umepitisha taarifa ya pamoja inayotoa wito wa kuimarisha ushirikiano wa pande nyingi na kujenga usimamizi duniani wenye usawa, licha ya Marekani kususia.
"Uenyekiti wa zamu wa G20 umefikia taarifa yenye umuhimu wa kupiga hatua ... ambayo itabadilisha jinsi Nchi za Kusini zinavyoshiriki na kutoa mchango katika uchumi wa dunia," Waziri wa Uhusiano na Ushirikiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini Ronald Lamola amesema baada ya taarifa hiyo ya pamoja kutangazwa.
Taarifa hiyo ya pamoja yenye vipengele 122, yenye kichwa cha "Mkutano wa Viongozi wa G20 Afrika Kusini: Taarifa ya Viongozi," inasisitiza haja ya kukabiliana na changamoto duniani kupitia ushirikiano wa pande nyingi na inatoa wito wa kutoa msaada mkubwa zaidi kwa nchi zinazoendelea ili kusukuma mbele ukuaji jumuishi na maendeleo endelevu.
Ingawa nchi wanachama wa G20 zimeunga mkono kwa kauli moja taarifa hiyo, Marekani, ambayo ilikataa kuhudhuria mkutano huo, imesema kwamba itakataa nyaraka yoyote ya matokeo itakayotolewa kama sehemu ya makubaliano ya G20 bila idhini yake.
Mvutano kati ya Afrika Kusini na Marekani umekuwa ukiongezeka tangu mwanzo wa mwaka huu. Serikali ya Marekani imesimamisha msaada wake kwa Afrika Kusini, ikidai kwamba Sheria ya kutwaa Ardhi, sheria ya mageuzi ya ardhi iliyosainiwa na Rais Cyril Ramaphosa mwezi Januari, mwaka huu "inawabagua" Waafrika Kusini weupe.
Wachambuzi wanasema kwamba Afrika Kusini iliikasirisha Marekani mwezi Desemba 2023 ilipowasilisha kesi mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ikiishitaki Israeli kwa kufanya "mauaji ya kimbari" dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza. Uhusiano kati ya nchi hizo mbili umeendelea kuwa na matatizo mwaka huu mzima.
Ikirejelea kile ilichokiita sera za kibaguzi za ardhi dhidi ya Waafrika Kusini weupe, Marekani kwanza ilipunguza msaada wa maendeleo kwa Afrika Kusini na baadaye kumfukuza balozi wa Afrika Kusini.
Mwezi Agosti, serikali ya Marekani iliweka ushuru wa asilimia 30 kwa bidhaa za Afrika Kusini, na kuifanya Afrika Kusini kuwa nchi ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara inayokabiliwa na kiwango cha juu zaidi cha ushuru kutoka Marekani.
Serikali ya Afrika Kusini imekataa shutuma hizo za Marekani ikisema kuwa zinakosa "ukweli wa mambo na kushindwa kutambua historia ndefu na yenye chungu ya ukoloni na ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini."
Katika mwaka huu mzima, Marekani imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kwamba hakuna maafisa wake watakaohudhuria mkutano huo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



