Lugha Nyingine
Kampuni ya China na EACOP zatoa mafunzo kwa vijana 80 wa Tanzania ili kuimarisha nguvukazi ya wenyeji
DAR ES SALAAM - Vijana 80 wa Tanzania wamehitimu kutoka programu ya mafunzo ya ufundi ya mwaka mmoja, ambayo ni hatua mpya katika juhudi za kuimarisha ujuzi wa nguvukazi ya wenyeji na kupanua fursa za kiuchumi, mmoja wa waandaaji wa programu hiyo amesema jana Jumapili.
Mpango huo, uliotekelezwa kwa pamoja na Kampuni ya Chuma ya Panyu Chu Kong (PCK), kampuni ya China, na Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), ulifanyika kwa ushirikiano na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi ya Tanzania (VETA), EACOP imesema katika taarifa.
EACOP ni bomba la kusafirisha mafuta ghafi lenye urefu wa kilomita 1,443 ambalo litasafirisha mafuta ghafi ya Uganda kutoka Kabaale-Hoima hadi peninsula ya Chongoleani karibu na Tanga, Tanzania, kwa ajili ya kusafirishwa kuuzwa kwenye masoko ya kimataifa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, programu hiyo ya mafunzo imetoa mafunzo ya vitendo katika nyanja nane za kiufundi, ambazo ni kuchomelea na kuunda miundo ya chuma, kuunganisha mabomba, kufunga mifumo ya umeme, uendeshaji wa mitambo, ufundi wa magari, uashi, upakaji rangi, na ufundi wa vifaa vya kielektroniki.
Wahitimu wametoka katika jamii zilizo karibu na njia ya bomba hilo la mafuta na wamepata mafunzo katika vituo vya VETA vilivyoko Moshi, Kilindi, na Shinyanga, imesema taarifa hiyo.
Programu hiyo iliyozinduliwa Januari 2025, ni sehemu ya mkakati wa maudhui ya ndani wa EACOP unaolenga kujenga nguvukazi yenye ushindani inayoweza kuendeleza sekta za viwanda na miundombinu za Tanzania zinazozidi kukua.
"Wahitimu wapya wamepokea vyeti vinavyotambuliwa kitaifa vilivyoandaliwa ili kuongeza uwezo wao wa kupata ajira na kuwawezesha kutoa mchango halisi katika maendeleo ya jamii," taarifa hiyo inasomeka.
Geofrey Mponda, kaimu meneja mkuu wa EACOP tawi la Tanzania, amesisitiza dhamira ya mradi huo kwa kukuza ujuzi kwa muda mrefu.
"Kuwekeza kwa watu ndiyo msingi wa dhamira ya EACOP," amesema, akiongeza kuwa kilomita 1,250 za njia za bomba hilo tayari zimeshafungwa na maendeleo ya jumla ya mradi huo yamefikia asilimia 74.
PCK, kampuni ya China iliyopewa kandarasi ya kutengeneza na kusambaza takriban kilomita 1,542 za njia za bomba hilo kwa ajili ya EACOP, ilikamilisha na kukabidhi katika awamu 16 kati ya 2023 na 2025, ikitimiza malengo yote muhimu bila kuchelewa, taarifa hiyo imeongeza.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



