Lugha Nyingine
Marekani na Ukraine yapunguza mpango wa amani kutoka vipengele 28 hadi 19

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio (kulia) na Andriy Yermak, mkuu wa ofisi ya rais ya Ukraine, wakikutana na waandishi wa habari kwenye Ujumbe wa Marekani kwa Umoja wa Mataifa na Mashirika Mengine ya Kimataifa mjini Geneva, Uswisi, Novemba 23, 2025. (Xinhua/Lian Yi)
WASHINGTON - Vyombo kadhaa vya habari vimeripoti jana Jumatatu kwamba Mpango wa amani wenye vipengele 28 uliopendekezwa na Marekani unaolenga kumaliza mgogoro wa Ukraine umepunguzwa hadi kuwa mfumokazi wenye vipengele 19 na Marekani na Ukraine mwishoni mwa wiki mjini Geneva.
Gazeti la The Washington Post lilimnukuu Oleksandr Bevz, afisa wa Ukraine aliyeshiriki kwenye mazungumzo hayo ya Geneva akisema kwamba "Vipengele vingi vyenye utata vimepunguzwa ukali au angalau kurekebishwa" ili kukaribia msimamo wa Ukraine au kupunguza madai kwa Ukraine.
Ameongeza kuwa tarehe ya mwisho ni Alhamisi, ambayo iliwekwa na Rais wa Marekani Donald Trump kwa makubaliano juu ya mpango huo wenye vipengele 28, sasa inaonekana kuwa yenye unyumbufu zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali.
"Sio hali ya dharura -- cha muhimu zaidi ni kukamilisha maandishi," amesema Bevz.
Naibu Waziri wa Kwanza wa Mambo ya Nje wa Ukraine Sergiy Kyslytsya ameliambia Gazeti la Financial Times kwamba rasimu hiyo mpya haina uhusiano mkubwa na toleo la awali la vipengele 28 lililovuja.
"Mambo machache sana yamebaki kutoka toleo la awali," amesema.
Rasimu hiyo mpya inaacha masuala yenye utata mkubwa zaidi kwa Rais Trump na mwenzake wa Ukraine Volodymyr Zelensky wanapaswa kuamua, kwa mujibu wa taarifa za vyombo mbalimbali vya habari.
Toleo la awali la vipengele 28 lingeitaka Ukraine kuachilia eneo la mashariki mwa Ukraine, kupunguza jeshi lake na kuachana na azma yake ya kujiunga na NATO. Kwa hivyo mpango huo ulivuka mistari kadhaa myekundu iliyodumu kwa muda mrefu ya Ukraine, ukisababisha ukosoaji kutoka Ukraine na kote Ulaya, kwa mujibu wa taarifa hizo.
Imeripotiwa kwamba katika mkutano huo wa Jumapili wa Geneva Marekani uliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio, Mjumbe Maalum wa Mashariki ya Kati Steve Witkoff na Waziri wa Jeshi Daniel Driscoll, huku ujumbe wa Ukraine ukiongozwa na mkuu wa ofisi ya Rais, Andriy Yermak.
Habari kutoka Newsweek zinasema kuwa, Ikulu ya Russia, Kremlin imesema haijapokea maelezo rasmi kutoka Geneva na haina mpango wa kufanya mazungumzo na maafisa wa Marekani wiki hii.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



