Lugha Nyingine
Wachapishaji vitabu wa Tanzania waunga mkono kuingizwa kwa lugha ya Kichina kwenye mtaala wa elimu
Uamuzi wa Tanzania wa kuingiza lugha ya Kichina kuwa somo la hiari katika mtaala wa elimu ya shule za msingi, umechochea msukumo mpya katika sekta ya uchapishaji vitabu kote nchini Tanzania.
Hatua hiyo inatarajiwa kuendeleza nguvu kazi ya baadaye inayoweza kushiriki kwa ufanisi zaidi katika biashara za pande mbili, utalii na mabadilishano ya kiutamaduni.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye mahojiano na Shirika la Habari la China, Xinhua, wadau wa sekta hiyo ya uchapishaji vitabu, wachapaji na wauza vitabu wamesema wanaanza kutafuta kununua vitabu vya kiada, vitabu vya hadithi, na miongozo kwa wanafunzi wa hatua ya awali. Baadhi ya vitabu vinatafutwa sana na shule na wazazi, kufuatia tangazo kuwa lugha ya Kichina itakuwa moja ya lugha za hiari kwenye mtihani wa taifa wa shule za msingi.
Mkuki Bgoya, mkurugenzi mkuu wa Kampuni ya Uchapishaji ya Mkuki na Nyota, amesema kuingizwa kwa lugha ya Kichina katika mtaala wa shule za msingi "ni fursa ambayo tumekuwa tukiisubiri."
Kampuni yake ya uchapishaji tayari imeshawahi kushirikiana na ubalozi wa China kutafsiri baadhi ya vitabu vyenye ushawishi nchini China kwa Kiswahili. "Toleo la Kiswahili linaweza kuwapa wasomaji wa Tanzania maarifa kuhusu uzoefu wa maendeleo ya China," amebainisha.
Hermes Damian, mwenyekiti wa Jumuiya ya Wachapishaji Tanzania, amevielezea vitabu kuwa ni "hifadhi ya mafanikio ya binadamu," akibainisha kuwa ushirikiano wa kimataifa, ukiwemo ule wa China, unaimarisha uwezo wa uchapishaji wa Tanzania.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



