Video mpya yahusisha wakati wa shambulizi la shule na ule wa shambulizi la jeshi la Marekani kwenye kambi ya karibu ya IRGC nchini Iran

(CRI Online) Machi 09, 2026

Kituo cha Televisheni cha CNN kimeripoti jana Jumapili kuwa, video mpya inaonesha shambulizi la anga la Marekani likilenga jengo moja kwenye kambi ya kikosi cha majini cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislam (IRGC) mjini Minab, Iran, karibu na shule ya msingi, ambako chombo cha habari cha taifa cha Iran kilisema kwamba wanafunzi zaidi ya 160 waliuawa Februari 28.

Video hiyo, iliyochapishwa mitandaoni na shirika la habari la Mehr News la Iran, ni ya kwanza kuonesha makombora yakishambulia eneo hilo na kuongeza idadi zaidi ya ushahidi unaoonesha kukinzana na madai yalitolewa hivi karibuni na Rais Donald Trump wa Marekani ya kuishutumu Iran juu ya tukio hilo.

Katika video hiyo, iliyopigwa kutoka eneo la karibu la ujenzi, kombora moja linalofanana na aina ya Tomahawk la Marekani linaweza kuonekana kabla ya kushambulia eneo lengwa ndani ya kambi ya kijeshi ya IRGC. Ripoti hiyo pia imebainisha kuwa Israel haitumii makombora hayo aina ya Tomahawk.

Mapema Jumamosi, Rais Trump aliilaumu Iran kuhusika na shambulizi hilo dhidi ya shule ya Minab, licha ya uchambuzi kutoka CNN na vyombo vingine vya habari.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha