UN yaonya usalama wa chakula nchini Sudan kuwa hatarini licha ya serikali kutoa uhakikisho

(CRI Online) Machi 09, 2026

Wakati vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan vikikaribia mwaka wa tatu, Umoja wa Mataifa umeonya kuwa mahitaji ya kibinadamu nchini humo yameongezeka, japo serikali ya Sudan imedai kuwa usambazaji wa chakula uko chini ya udhibiti, hali ambayo inazua wasiwasi juu ya mustakabali wa usalama wa chakula wa nchi hiyo.

Mpango wa Msaada wa Kibinadamu wa 2026 wa Umoja wa Mataifa umekadiria kuwa mwaka huu watu milioni 33.7 nchini Sudan watahitaji msaada, ikiwa ni ongezeko la milioni 3.3 kutoka mwaka 2025.

Umoja huo umehusisha ongezeko hilo la mahitaji ya msaada na watu kukimbia makazi yao, kukatika kwa mnyororo wa usambazaji, kuongezeka kwa bei za bidhaa, kupungua kwa uzalishaji wa kilimo katika maeneo yaliyoathiriwa na mapigano, vilevile kuzorota kwa hali ya huduma ya afya, maji na usafi, huku operesheni ya utoaji wa misaada ikikwamishwa na uhaba wa fedha na changamoto za ufikiaji.

UN inakadiria kuwa dola za kimarekani bilioni 2.8 zinahitajika kwa ajili ya operesheni ya misaada ya kibinadamu mwaka huu ili kufikia watu milioni 20.4 miongoni mwa walio katika mazingira magumu zaidi. Mashirika ya kutoa misaada yanaonya kuwa mapengo ya ufadhili wa fedha yanaweza kuwaacha watu wasiopungua milioni 14.2 bila msaada.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha