Waziri wa Mambo ya Nje wa China atoa wito wa kusimamishwa vita katika eneo la Ghuba haraka iwezekanavyo

(CRI Online) Machi 10, 2026

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Bw. Wang Yi amesema, kipaumbele cha juu zaidi kwa sasa ni kufikia usimamishaji vita haraka iwezekanavyo, akiongeza kuwa China inapongeza wito wa wakati wote wa kutaka mazungumzo kutoka kwa mataifa ya Ghuba.

Bw. Wang, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China, ametoa kauli hiyo katika mazungumzo kwa njia ya simu na mwenzake wa Kuwait, Jarrah Jaber Al-Ahmad Al-Sabah.

Bw. Wang Yi amesema China siku zote inaunga mkono kutatua migogoro kwa njia za kisiasa na kidiplomasia, akisisitiza kuwa mapigano yanayoendelea ni vita ambavyo havikupaswa kutokea na havitumikii maslahi ya upande wowote.

Bw. Wang amesema, Marekani na Israel zilianzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran bila idhini ya Umoja wa Mataifa, wakati mazungumzo kati ya Iran na Marekani yalikuwa bado yakiendelea, kitendo ambacho ni ukiukwaji dhahiri wa sheria za kimataifa.

Bw. Wang Yi amesema, mjumbe maalum wa serikali ya China anayeshughulikia masuala ya Mashariki ya Kati ameshaondoka kwenda kwenye kanda hiyo kupatanisha na ataimarisha mawasiliano na Kuwait na nchi nyingine.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha