Lugha Nyingine
Waziri wa Mambo ya Nje wa China ahimiza kusimamishwa vita Mashariki ya Kati
Waziri wa Mambo ya Nje wa China Bw. Wang Yi amesema kwamba China inatoa wito wa kusimamishwa vita mara moja katika eneo la Mashariki ya Kati na juhudi za kuelekea suluhu ya kisiasa, na inaziunga mkono nchi za Ghuba katika kuchukua mustakabali wa eneo hilo mikononi mwao.
Wang, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China, ameyasema hayo jana Jumanne kwenye mazungumzo kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa Qatar ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani.
Wang amesema, China ikiwa ni mjumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, siku zote imekuwa ikifuata kanuni na kushikilia haki na usawa katika masuala ya kimataifa.
Amesema, operesheni za kijeshi zinazofanywa na Marekani na Israeli dhidi ya Iran, bila idhini ya Baraza la Usalama, dhahiri zinakiuka madhumuni na kanuni za Mkataba wa Umoja wa Mataifa, pamoja na kanuni za kimsingi zinazoongoza uhusiano wa kimataifa.
"China haikubali upanuzi wa wigo wa mashambulizi na inalaani mashambulizi holela dhidi ya raia na maeneo lengwa yasiyo ya kijeshi,” Wang amesema, akiongeza kuwa mamlaka huru, usalama na ukamilifu wa ardhi wa mataifa ya Ghuba ya Kiarabu lazima viheshimiwe.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



