Lugha Nyingine
Mashambulizi ya Israeli nchini Lebanon yaripotiwa kuua watu 570, karibu 760,000 wakimbia makazi yao
BEIRUT - Idadi ya vifo kutokana na mashambulizi yanayoendelea ya Israeli dhidi ya Lebanon imeongezeka hadi 570, huku wengine 1,444 wakijeruhiwa tangu kupamba moto kwa mashambulizi hayo kuanze Machi 2, takwimu zilizotolewa jana Jumanne na Kitengo cha Usimamizi wa Hatari za Maafa katika Baraza la Mawaziri la Lebanon zinaonyesha.
Mgogoro huo umesababisha watu wengi kukimbia makazi yao katika sehemu mbalimbali za nchi hiyo. Watu takriban 759,300 wamesajiliwa kuwa wamekimbia makazi yao, kwa mujibu wa takwimu hizo za serikali.
Mamlaka zimesema watu 122,600 waliokimbia makazi yao kwa sasa wanaishi kwenye makazi 580 yaliyoandaliwa katika maeneo mbalimbali ili kuhifadhi familia zilizolazimishwa kukimbia makazi yao wakati huu ambapo kuna uhasama unaoendelea.
Shirika la Habari la Taifa la Lebanon limeripoti, wakati huo huo, Israel imefanya mashambulizi matatu ya anga katika vitongoji vya kusini mwa Beirut jana Jumanne alasiri, na kuendeleza mashambulizi katika maeneo kadhaa kusini mwa Lebanon.
Hezbollah imesema ilirusha makombora kutoka Lebanon kuelekea Israeli mapema Machi 2 kwa mara ya kwanza tangu usimamishaji mapigano uliotangazwa Novemba 27, 2024. Hatua hiyo ilisababisha serikali ya Lebanon kupiga marufuku shughuli za usalama na kijeshi za kundi hilo, ikilipa idhini ya kazi ya kisiasa pekee na kulitaka likabidhi silaha zake.
Jeshi la Israeli lilisema limeanzisha kile lilichokielezea kuwa ni "kampeni ya kijeshi ya mashambulizi" dhidi ya Hezbollah, likifanya mashambulizi makubwa ya anga katika maeneo mengi ya Lebanon na operesheni za ardhini karibu na mpaka. Pia limewapa tahadhari wakazi kuhama maeneo ya kusini mwa Mto Litani na vitongoji vya kusini mwa Beirut.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



