Lugha Nyingine
Misri yapandisha bei za mafuta kutokana na mashinikizo ya soko la nishati duniani

Watu wakijaza mafuta magari yao kwenye kituo cha mafuta mjini Cairo, Misri, Machi 10, 2026. (Xinhua/Ahmed Gomaa)
CAIRO - Wizara ya Petroli na Rasilimali za Madini ya Misri imesema katika taarifa yake kwamba Misri imepandisha bei za mafuta nchini humo mapema jana Jumanne, ikirejelea hali isiyo kawaida katika masoko ya nishati duniani.
Bei hizo zimeongezeka kwa asilimia takriban 14 hadi 17 katika bidhaa mbalimbali muhimu za petroli.
Taarifa hiyo inaonesha kuwa, bei ya petroli ya oktanu 95 imepanda hadi pauni 24 za Misri (dola 0.45 za Marekani) kwa lita kutoka pauni 21, petroli ya oktanu 92 hadi pauni 22.25 kutoka pauni 19.25, petroli ya oktanu 80 hadi pauni 20.75 kutoka pauni 17.75, na dizeli hadi pauni 20.5 kutoka pauni 17.5.
Wakati huo huo, bei ya gesi asilia kwa magari iliyoshinikizwa imeongezeka hadi pauni 13 kwa kila mita ya ujazo kutoka pauni 10, taarifa hiyo imesema.
Wizara hiyo imesema kwamba bei hizo mpya zimeanza kutumika saa 9 jioni kwa saa za Misri (0100 GMT) siku hiyo ya Jumanne.
Wizara hiyo imehusisha marekebisho hayo ya bei na "hali isiyo kawaida inayotokana na maendeleo ya siasa za kijiografia katika Mashariki ya Kati na athari zake za moja kwa moja katika masoko ya nishati duniani," hali ambayo wizara hiyo imesema imeongeza kwa kiasi kikubwa gharama za uagizaji na uzalishaji wa nchini.
“Mvurugiko katika minyororo ya usambazaji, viwango vya hatari vinavyozidi kuongezeka, na gharama kubwa zaidi za usafirishaji wa baharini na bima vimesababisha ongezeko kubwa la bei za mafuta ghafi na bidhaa za petroli duniani, zikifikia viwango ambavyo havijawahi kuonekana kwa miaka mingi,” wizara hiyo imeongeza.
Taarifa hiyo imesema katika kukabiliana na changamoto hizo, serikali ya Misri inaendelea na juhudi za kuongeza uzalishaji wa nchini na kupanua utafutaji wa mafuta na gesi ili kupunguza gharama ya uagizaji ya Misri.
Imeongeza kuwa mamlaka zinafuatilia kwa karibu maendeleo ya soko na gharama ili kuhakikisha uendelevu wa usambazaji wa petroli na gesi kwa raia na sekta zote za nchi, wakati huohuo ikidumisha usalama wa nishati na utulivu katika soko la nchini.
Ongezeko hilo la bei ya mafuta ya nchini Misri linatokea huku kukiwa na mgogoro unaoendelea unaohusisha Marekani, Israel na Iran, ambao umeweka kivuli chake katika eneo la Ghuba na kuathiri masoko ya mafuta na gesi duniani.

Watu wakijaza mafuta vyombo vyao vya usafiri kwenye kituo cha mafuta mjini Cairo, Misri, Machi 10, 2026. (Xinhua/Ahmed Gomaa)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



