Ripoti zaeleza Marekani ilihamisha mfumo wa makombora wa THAAD kutoka Korea Kusini kwenda Mashariki ya Kati

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 12, 2026

Shirika la Habari la Korea Kusini, SBS limeripoti jana Jumatano kwamba limepata video inayoonesha kuwa Mfumo wa Kukinga dhidi ya Makombora wa THAAD wa Marekani uliokuwa umewekwa kwenye kambi ya Seongju katika Jimbo la Gyeongsang Kaskazini, Korea Kusini ulisafirishwa kutoka kambi hiyo hadi eneo la Mashariki ya Kati mapema mwezi huu wa Machi.

Video hiyo, iliyoripotiwa kurekodiwa Machi 3 kwenye barabara ya vijijini karibu na kambi hiyo ya kijeshi ya Marekani nchini Korea Kusini, inaonyesha malori kadhaa makubwa yaliyofunikwa kwa turubai yakipita mfululizo kwa kipindi cha dakika zaidi ya 10.

Ripoti hiyo inasema kwamba vifyatuaji makombora sita vya mfumo huo wa THAAD vilitambuliwa kuwa miongoni mwa vifaa hivyo vilivyokuwa vikisafirishwa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo kambi hiyo ya Seongju ina mfumo wa ufanyaji kazi wa THAAD wenye vifyatua makombora sita, ikimaanisha kwamba vifyatua makombora vyote vya mfumo huo wa THAAD sasa vimeondolewa kwenye kambi hiyo.

Ripoti ya Washington Post ya Machi 9, imesema kuwa Marekani inahamisha baadhi ya mifumo ya THAAD iliyokuwa imewekwa Korea Kusini hadi Mashariki ya Kati. Ripoti hiyo imenukuu maafisa wawili wa serikali ya Marekani wakisema kwamba sambamba na mfumo huo wa THAAD, jeshi la Marekani pia linapeleka Mfumo wa Patriot wa Kuzuia Makombora (Patriot interceptor) kutoka eneo la Bahari ya Hindi na Pasifiki (Indo-Pacific) na maeneo mengine.

Kwa mujibu wa Ikulu ya Korea Kusini, Blue House, Rais wa Korea Kusini Lee Jae-myung alisema kwenye mkutano wa baraza la mawaziri wa Machi 10 kwamba serikali ya Korea Kusini inapinga jeshi la Marekani kupelekwa baadhi ya silaha za ulinzi wa anga, lakini ukweli halisi ni kwamba kwa maoni ya Korea Kusini ni vigumu kutekeleza.

(Wahariri wa tovuti:Zhao Jian)

Picha