Kampuni za umiliki wa mtu mmoja zinazowezeshwa na wakala wa AI zawa mada moto katika "mikutano mikuu miwili" ya China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 12, 2026

Fundi (kulia) akizungumza na mtumiaji baada ya kuweka wakala wa AI wa chanzo wazi OpenClaw kwenye kompyuta mjini Nanjing, Mkoa wa Jiangsu, Mashariki mwa China, Machi 11, 2026. (Xinhua/Ji Chunpeng)

Fundi (kulia) akizungumza na mtumiaji baada ya kuweka wakala wa AI wa chanzo wazi OpenClaw kwenye kompyuta mjini Nanjing, Mkoa wa Jiangsu, Mashariki mwa China, Machi 11, 2026. (Xinhua/Ji Chunpeng)

BEIJING -- "Kufuga kambakoche" (Raising lobster) na kampuni za umiliki wa mtu mmoja (OPCs), ambazo zimezua mijadala mikali katika jamii ya AI ya China na miongoni mwa umma, pia ni mada moto katika "mikutano mikuu miwili" inayoendelea ya nchi hiyo mwaka huu.

Istilahi "kufuga kambakoche" ilitokana na wakala wa AI wa chanzo wazi (open-source) OpenClaw, ambaye anatumia kambakoche mwekundu kama utambulisho wake. Tangu wakati huo imekuwa neno maarufu linalotumiwa na watumiaji wa China kueleza mchakato wa kuweka kwenye kompyuta na kufunza msaidizi huyu wa AI.

Katika mji ambao ni kituo cha teknolojia wa kusini mwa China wa Shenzhen, shauku hiyo haiwezekani kuikosa -- mamia ya wapenzi wamekuwa wakijipanga foleni nje ya makao makuu ya kampuni ya teknolojia ya Tencent ili kuwekewa wakala huyo kwenye kompyuta zao.

Kampuni nyingi za teknolojia za China tangu wakati huo zimeingia kwenye wimbi hilo, zikianzisha "kambakoche" wao wenyewe. Kampuni ya Tencent imetoa QClaw, Minimax imetoa MaxClaw, Moonshot AI imetoa KimiClaw, na Alibaba imejiunga na uhondo huo kwa kuanzisha CoPaw.

Ding Hong, mshauri wa kisiasa wa kitaifa na mwanataaluma wa Akademia ya Sayansi ya China, amesema kuwa kuibuka kwa mawakala hao wa AI kunawezesha watu wa kawaida wasio na ujuzi wa kufunza programu za kompyuta (coding) kutengeneza katika muda mfupi programu zinazoweza kutumika.

Biashara "zinazowezeshwa na mfumo wa wakala wa AI" zinajikita katika kujenga mwingiliano wa muda mrefu na mawakala wa AI ili kujenga kumbukumbu zao na mantiki ya kiutendaji. Mchakato huo hatua kwa hatua unawageuza mawakala hao kuwa "wasaidizi wakuu" wenye uwezo wa kusimamia mitiririko ya kazi, kama vile kushughulikia mazungumzo, utumaji wa barua pepe, na ubunifu wa maudhui. Watu binafsi wanaweza kutumia kikamilifu mawakala hawa wa AI kukamilisha kazi ambazo kwa kawaida zingehitaji timu nzima.

"Hii imesababisha kuibuka kwa mfumo mpya kabisa wa OPC (kampuni ya umiliki wa mtu mmoja), na kuwa aina mpya ya uchumi wa AI wenye hamasa. OPCs zitakuwa wimbi la muda mrefu linaloakisi mageuzi makubwa katika mgawanyo wa kazi na vitengo vya msingi vya shughuli za kiuchumi," Ding ameongeza.

Ripoti ya kazi ya serikali ya mwaka huu ya China imesisitiza hitaji la kuunda "aina mpya za uchumi wa teknolojia za kisasa" kwa mara ya kwanza. Inatoa wito kwa ajili ya kukuza matumizi ya haraka ya vifaa vya AI vya kizazi kipya na mawakala wa AI, matumizi makubwa ya kibiashara ya AI katika sekta na nyanja muhimu, na ukuzaji wa aina na mifumo mipya ya biashara yenye asili ya AI (AI-native).

"AI Plus" pia ni sehemu muhimu katika muswada wa mwongozo wa Mpango wa 15 wa Miaka Mitano wa China (2026-2030), ambao kwa sasa unajadiliwa katika "mikutano mikuu miwili."

Chini ya mpango wa kimkakati wa ngazi ya juu wa China, wajasiriamali wana uharaka wa kubadilika kuendana na matumizi ya teknolojia za kisasa, wakiwa na shauku ya kukamata fursa za kibiashara zinazojitokeza, huku serikali za mitaa zikiwa tayari kuchochea dharura hii ya kibiashara.

Hata hivyo, kama aina mpya kabisa ya kampuni, OPCs bado zinakabiliwa na matatizo kama vile umiliki usio dhahiri wa hakimiliki za maudhui yanayotengenezwa na AI.

Qi Xiangdong, mshauri wa kisiasa wa kitaifa wa China na mwenyekiti wa kampuni ya usalama wa mtandao ya QAX Group, pia ameonya kuwa kutoa ruhusa ya data kupita kiasi kwa mawakala wa AI kunaleta hatari za kiusalama, zikiwemo za uvujaji wa usalama wa data, ulinzi usiotosha dhidi ya mashambulizi ya mtandaoni, na masuala ya usalama katika huduma za umma za kidijitali.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha