Lugha Nyingine
Kiongozi Mkuu mpya wa Iran ahimiza kuendelea kufungwa Mlango Bahari wa Hormuz, aahidi kufungua mistari mipya ya mbele ya vita

Picha hii kutoka waraka ikimwonesha Mojtaba Khamenei, kiongozi mkuu mpya wa Iran. (Xinhua)
TEHRAN - Kiongozi mkuu mpya wa Iran Mojtaba Khamenei jana Alhamisi katika ujumbe wake wa kwanza uliochapishwa kwenye tovuti yake tangu tangazo la Jumapili wiki hii la kuteuliwa kwake kuwa kiongozi mkuu wa Iran, amehimiza kuendelea kufungwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz na kuahidi kufungua mistari mipya ya mbele katika mgogoro kati ya nchi yake na Marekani na Israeli.
"Mahitaji ya watu ni mwendelezo wa ulinzi wenye ufanisi na wa kutoa majuto. Pia, kisawazishi cha kuzuia Mlango Bahari wa Hormuz lazima kiendelee kutumika," Khamenei amesema, akihutubia watu na vikosi vya jeshi la nchi hiyo.
Amesema utafiti umefanywa juu ya kufungua mistari mingine ya vita ambako adui hana uzoefu mwingi na atakuwa dhaifu sana, na mistari hii itafunguliwa kama hali ya vita itaendelea na kwenye msingi wa kuzingatia maslahi.
Khamenei ametoa salamu za rambirambi kutokana na "kifo cha kishujaa cha kutia simanzi" cha baba yake, Kiongozi Mkuu wa zamani Ali Khamenei, akisema amefahamu kuhusu uamuzi wa Baraza la Wataalamu wa kumchagua kuwa kiongozi mpya wa Iran, kama Wairani wengine, kupitia televisheni ya IRIB inayoendeshwa na serikali ya Iran.
Kiongozi huyo mkuu mpya amevisifu vikosi "shujaa" vya jeshi la nchi hiyo, ambavyo "vimezuia njia za maadui kwa mapigo yao makali, na vimeondoa kujidanganya kwao kwamba wanaweza kutawala au pengine kuigawanya Iran."
Ameapa kulipa kisasi kufuatia "mashujaa wa Iran waliomwaga damu," na akasema Iran itatafuta fidia kutoka kwa "maadui" wake. Kama ikikataliwa, "tutachukua mali yao kadri tutakavyoamua, na kama hilo lisipowezekana, tutaharibu kiasi chenye thamani sawa cha mali yao," amesema.
Khamenei amesema Iran ina nia ya kuwa na uhusiano "mzuri na wa kiujenzi" na nchi zote 15 ambazo inapakana nazo kwenye mipaka ya ardhini au majini. Hata hivyo, amesema kutokana na uwepo wa vituo vya kijeshi na kifedha vya "adui" katika baadhi ya nchi hizo, mashambulizi ya Iran kwenye vituo hivyo yataendelea bila kushambulia majirani wenyewe.
Ameshauri majirani wa Iran kufunga vituo hivyo vya kijeshi vya Marekani katika ardhi zao haraka iwezekanavyo, "kwani bila shaka wameshagundua kufikia sasa kwamba dai la Marekani la kuimarisha usalama na amani halikuwa ni chochote zaidi ya uwongo."
Februari 28, Israeli na Marekani zilianzisha mashambulizi ya pamoja dhidi ya Tehran na miji mingine kadhaa ya Iran, na kumuua Kiongozi Mkuu wa Iran wa wakati huo Ali Khamenei, pamoja na makamanda waandamizi wa kijeshi na raia. Iran ilijibu kwa kuanzisha mawimbi ya mashambulizi ya makombora na droni kuilenga Israeli na vituo na mali za Marekani katika Mashariki ya Kati.

Wanajeshi wa Iran wakifanya doria kwenye Mlango Bahari wa Hormuz kusini mwa Iran, Aprili 30, 2019. (Xinhua/Ahmad Halabisaz)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



