Lugha Nyingine
Israel yalenga jengo katikati mwa Beirut katika wimbi jipya la mashambulizi
BEIRUT - Jeshi la Israel limetangaza jana Alhamisi alasiri kwamba lilifanya mfululizo mpya wa mashambulizi ya anga mjini Beirut, Lebanon yakilenga maeneo lengwa ya Hezbollah.
Tahadhari zilitolewa zikihimiza wakazi kuondoka kwenye majengo mahsusi katika maeneo ya Bachoura na Zkak al-Blat kabla ya mashambulizi hayo kufanywa. Jengo lililolengwa katika eneo la Zkak al-Blat ni makao ya tawi la Al-Qard Al-Hassan, ambalo Israeli inadai Hezbollah inalitumia kama mkono wa kifedha kufadhili ununuzi wa silaha na kulipa wapiganaji wake.
Tahadhari na mashambulizi hayo yaliyofuata yalisababisha hofu miongoni mwa wakazi na familia zilizokimbia makazi yao ambazo zilikuwa zimekimbia mashambulizi ya awali ya Israeli na kukimbilia katikati mwa Beirut.
Wakati huo huo, Wizara ya Afya ya Umma ya Lebanon imeripoti jana Alhamisi kwamba idadi ya vifo kutokana na mashambulizi ya Israeli nchini Lebanon imeongezeka hadi 687 tangu Machi 2, huku majeruhi wakiwa 1,774.
Wizara hiyo imeongeza kuwa idadi ya wahudumu wa afya waliouawa imefikia 18, huku wengine 45 wakijeruhiwa.
Pia siku hiyo ya Alhamisi, Waziri Mkuu wa Lebanon Nawaf Salam alisema serikali inafanya kazi ya kusimamisha vita hivyo vinavyoendelea na kuhakikisha wakazi waliokimbia makazi yao wanarudi salama.
Pia amezishukuru jamii za Lebanon kwa kuzihifadhi familia zilizokimbia makazi yao na kuelezea shukrani kwa nchi rafiki kwa kutoa msaada wa kibinadamu ili kupunguza mateso ya raia.
Hezbollah ilitangaza kurusha roketi kutoka Lebanon kuelekea Israel alfajiri ya Machi 2 kwa mara ya kwanza tangu kutangazwa kusimamishwa kwa mapigano Novemba 27, 2024.
Israel baadaye ilianzisha kile ilichokielezea kuwa ni "kampeni ya kijeshi ya mashambulizi" dhidi ya kundi hilo, yakiwemo mashambulizi makali ya anga yakilenga vitongoji vya kusini vya Beirut na maeneo ya kusini na mashariki mwa Lebanon, vilevile mashambulizi ya ardhini.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



