Lugha Nyingine
ChinaVumbuzi | Askari polisi roboti wa usalama barabarani aanza kufanya kazi katika Mji wa Shenzhen, kusini mwa China

Picha iliyopigwa kwa simu ikionesha askari polisi roboti wa usalama barabarani akiongoza vyombo vya usafiri kwenye makutano ya barabara katika Eneo la Longgang, Shenzhen, Mkoa wa Guangdong, Kusini mwa China, Machi 6, 2026. (Polisi wa Usalama Barabarani wa Shenzhen/Xinhua)
SHENZHEN – Roboti inayoleta taswira ya siku za baadaye kwa sasa inaongoza vyombo vya usafiri barabarani katika Mji wa Shenzhen, mji ambao ni kituo cha teknolojia katika Mkoa wa Guangdong, kusini mwa China.
Katika mtaa wa Bantian wa Eneo lake la Longgang, roboti iliyovalia mavazi yenye nembo ya "Polisi wa Usalama Barabarani wa Shenzhen" imeanza rasmi kuwa "kazini" tangu Machi 6, ikisimamia msongamano wa asubuhi kwenye makutano ya barabara. Baada ya kuboreshwa kutoka jukumu lake la awali la kuwa muenezaji elimu ya usalama kando ya barabara, askari polisi huyu roboti wa usalama barabarani sasa anasimama imara kwenye jukwaa katikati ya makutano ya barabara.
Tofauti na mabango ya jadi ya alama za barabarani yasiyokuwa na mijongeo ya kiishara, roboti hiyo hutumia moduli za viungo zenye usahihi wa kiwango cha juu wa kufanya ishara za kawaida za trafiki, kama vile kuashiria kwenda mbele, kukata kona na kusimama, kwa wakati na hatua halisi sawa na taa za barabarani.
Mfumo wake wa AI wa utambuzi wa mazingira halisi unairuhusu "kuitazama" njia panda kwa makini. Wakati inapobaini ukiukaji wa taratibu za barabarani kama vile mwendesha skuta ya umeme asiyevaa kofia ngumu au gari linalosimama kupita mstari, mara moja hupiga filimbi ya onyo na kufanya ishara ya mkono ya kurekebisha kosa husika.
Uvumbuzi huu unaendana kiasili na mji huo wa Shenzhen, ambao unachukuliwa sana kuwa "Mji mkuu wa Teknolojia" wa China. Ripoti ya kazi ya serikali ya mji huo kwa mwaka huu inasisitiza hadhi yake ya kuwa kiongozi wa kitaifa katika uvumbuzi, huku uwekezaji wake katika utafiti na maendeleo ukifikia asilimia 6.67, kiwango cha juu zaidi miongoni mwa miji yote ya China, na uwekezaji wa kampuni katika utafiti na maendeleo unachukua asilimia zaidi ya 93 ya jumla ya Shenzhen.
Uwekaji huu wa askari polisi roboti wa usalama barabarani ni sehemu ya mwelekeo wa kitaifa wa China katika sekta ya mambo ya roboti zenye umbo la binadamu inayokua kwa kasi. Tangu mwaka jana, miji mikubwa kadhaa nchini China, kama vile Shanghai, Hangzhou na Chengdu, imeanza kutazama namna ya kutumia maafisa wa polisi roboti katika majukumu ya kila siku.

Picha iliyopigwa kwa simu ikionesha askari polisi roboti wa usalama barabarani akiwa kwenye makutano ya barabara katika Eneo la Longgang, Shenzhen, Mkoa wa Guangdong, Kusini mwa China, Machi 6, 2026. (Polisi ya Usafiri ya Shenzhen/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



