Lugha Nyingine
Sera ya China ya kuruhusu bidhaa za Afrika kuingia bila kutozwa ushuru yatarajiwa kuongeza mauzo ya nje, alisema mtaalamu
HARARE - Mchambuzi wa uchumi na mtoa maoni ya kisiasa wa Zimbabwe Dereck Goto amesema sera ya utozaji ushuru-sifuri ya China kwa bidhaa kutoka nchi 53 za Afrika itatoa fursa za kimageuzi kwa wauzaji nje wa Afrika.
Akizungumza na Shirika la Habari la China, Xinhua siku ya Ijumaa, Goto amesema sera hiyo inawakilisha mabadiliko makubwa ya kimuundo katika uhusiano wa kibiashara kati ya China na nchi za Afrika.
"Kwa nchi kama vile Zimbabwe, matokeo yake yana uwezekano mkubwa wa kuwa ya kimageuzi. Itaongeza uwezo wa kushindana wa mauzo ya nje ya Zimbabwe kama vile bidhaa za bustani katika soko la China," Goto amesema.
China ilitangaza mwezi wa Februari kwamba itatekeleza kikamilifu sera ya utozaji ushuru-sifuri kwa nchi 53 za Afrika zenye uhusiano wa kidiplomasia na China, kuanzia Mei 1.
Goto alisema sera hiyo pia itatoa motisha kwa upanuzi wa uzalishaji na ukuaji wa aina za bidhaa na mazao. Amesema, wauzaji nje wa Zimbabwe wataweza kuweka bei kiushindani zaidi kuliko wauzaji bidhaa kutoka maeneo mengine.
Kwa mujibu wa Goto, sera hiyo inaendana na mfumo mpana wa ushirikiano kati ya China na Afrika chini ya Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika.
"Katika miongo miwili iliyopita, mfumo huo umehama kwa hatua madhubuti kuelekea biashara, uungaji mkono wa maendeleo ya viwanda na maendeleo ya miundombinu. Ufikiaji soko wa bila kutozwa ushuru unakamilisha shoroba za miundombinu, miradi ya usafirishaji na maeneo maalum ya viwanda ambavyo tayari vimeendelezwa kupitia ushirikiano kati ya China na Afrika," amesema.
Goto alisema, Zimbabwe lazima ihakikishe utayari wa upande wa utoaji. Wauzaji nje lazima wakidhi vigezo vya usafi wa mimea, vigezo vya ubora na mahitaji ya usafirishaji ya China. Bila sera ya viwanda iliyoratibiwa na uungaji mkono wa mauzo ya nje, fursa hiyo inaweza kubaki bila kutumika kikamilifu.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



