Lugha Nyingine
China na Marekani zafanya mazungumzo ya wazi, ya kina, na ya kiujenzi juu ya masuala ya uchumi na biashara

Naibu Waziri Mkuu wa China He Lifeng, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), akisalimiana na Waziri wa Fedha wa Marekani Scott Bessent kabla ya mazungumzo yao mjini Paris, Ufaransa, Machi 15, 2026. (Xinhua/Peng Ziyang)
PARIS - Wajumbe wa China na Marekani wakiongozwa na Naibu Waziri Mkuu wa China He Lifeng na Waziri wa Fedha wa Marekani Scott Bessent mtawalia, wamefanya mazungumzo ya wazi, ya kina na ya kiujenzi mjini Parisi kuanzia Jumapili hadi Jumatatu juu ya masuala ya uchumi na biashara yanayofuatiliwa na pande zote mbili, ikiwemo mipango ya ushuru, kuhimiza biashara na uwekezaji wa pande mbili, na kudumisha maafikiano ya mashauriano yaliyopo sasa.
Kwenye mazungumzo hayo, ambayo yanaongozwa na maafikiano muhimu yaliyofikiwa na viongozi wakuu wa nchi hizo, pande hizo mbili zimefikia maafikiano mapya na kukubaliana kuendelea na mashauriano.
"Hivi karibuni, Mahakama Kuu ya Marekani iliamua kwamba ushuru uliowekwa na serikali ya Marekani kwa mujibu wa Sheria ya Dharura ya Kimataifa ya Mamlaka za Kiuchumi ulikuwa kinyume cha sheria," amesema He kwenye mkutano huo, akibainisha kuwa baadaye, upande wa Marekani uliweka ushuru wa ziada wa asilimia 10 kwa bidhaa za kuagizwa kutoka washirika wake wote wa kibiashara chini ya Kifungu cha 122 cha Sheria ya Biashara ya 1974, na kwa mfululizo ulianzisha hatua hasi kuhusu China, zikiwemo za chunguzi za Kifungu cha 301, vikwazo kwa kampuni na vizuizi vya upatikanaji wa soko.
He amesema China inatarajia Marekani kusonga mbele katika mwelekeo sawa, kufuata maafikiano muhimu yaliyofikiwa na viongozi wakuu wa nchi hizo mbili, kupanua maeneo ya ushirikiano na kupunguza matatizo, ili kuhimiza maendeleo mazuri, imara na endelevu ya uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Marekani.
Pande hizo mbili zimekubaliana kutafiti namna ya kuanzisha utaratibu wa ushirikiano wa kuhimiza biashara na uwekezaji wa pande mbili, kuendelea kutumia vyema utaratibu wa mashauriano ya kiuchumi na kibiashara kati ya China na Marekani, kuimarisha mazungumzo na mawasiliano, kusimamia ipasavyo tofauti kati zao, kupanua ushirikiano wa kivitendo, na kuhimiza maendeleo endelevu, thabiti na mazuri ya uhusiano wa kiuchumi na kibiashara wa pande mbili.
"Mada zilizojadiliwa kati ya pande mbili zilijumuisha viwango vya ushuru wa pande mbili katika mazingira mapya, uwezekano wa kupanuliwa zaidi kwa mipango inayohusiana na ushuru wa pande mbili na hatua husika zisizo za ushuru," amesema Li Chenggang, mwakilishi wa biashara ya kimataifa wa China katika Wizara ya Biashara ya China ambaye pia ni naibu waziri wa biashara, kwenye mkutano wa kutoa taarifa kufuatia duru hiyo mpya ya mazungumzo kuhusu uchumi na biashara kati ya China na Marekani.
Kuhusu hatua za vizuizi zilizoanzishwa na upande wa Marekani juu ya biashara na uwekezaji wa China, hasa chunguzi mbili za hivi karibuni za Kifungu cha 301 zinazohusisha China, Li amesema kwamba China imewasilisha kwa maneno makali msimamo wake na imeeleza wasiwasi mkubwa wakati wa mashauriano hayo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



