Lugha Nyingine
Washirika wa Ulaya wapinga wito wa Trump wa jukumu la kijeshi kwenye Mlango Bahari wa Hormuz

Watoto wakicheza kando ya ufukwe katika Kijiji cha Kumzar, Oman, Februari 19, 2025. (Xinhua/Wang Qiang)
BERLIN - Nchi kadha wa kadha za Ulaya na Umoja wa Ulaya (EU) zimeelezea hali ya kusitasita au kupinga moja kwa moja wito wa Rais wa Marekani Donald Trump wa kuzitaka zibebe jukumu la kijeshi ili kuhakikisha usafirishaji salama kwenye Mlango wa Hormuz.
Wakisisitiza hitaji la utatuzi wa kidiplomasia na kuonya kutoufanya mgogoro huo wa kikanda kupamba moto, viongozi wa Ulaya jana Jumatatu wamesisitiza kwamba mgogoro huo wa sasa haupaswi kubadilika kuwa jukumu la NATO au kulivuta bara hilo katika vita pana.
Chansela wa Ujerumani Friedrich Merz amekataa kuhusika kwa jeshi katika kulinda meli za mafuta kwenye mlango bahari huo, akisisitiza kwamba NATO ni "jumuiya ya kujihami" siyo "jumuiya ya kuingilia kati."
Merz amesema Ujerumani haitashiriki katika hatua za kijeshi za kuhakikisha uhuru wa usafirishaji baharini kama mgogoro huo bado unaendelea, na ameongeza kuwa mpaka sasa haujatolewa mpango wa kufaa kwa vitendo vya kufanyika.

Chansela wa Ujerumani Friedrich Merz akizungumza kwenye mkutano wake na waandishi wa habari wa majira ya joto mjini Berlin, Ujerumani, Julai 18, 2025. (Xinhua/Li Hanlin)
Maneno aliyosema yameitikiwa mjini Brussels na Kaja Kallas, Mkuu wa Sera za Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya (EU). Baada ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa EU, Kallas amesema umoja huo hauna nia ya kupanua jukumu la sasa la vikosi vya majini vya EU la "Aspides" hadi kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz.
"Tunatafuta sasa mpango wa kidiplomasia kwa utatuzi wa hali ya Mlango-Bahari wa Hormuz," amesema na kuongeza, "Hivi si vita vya Ulaya."

Mkuu wa sera za mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Brussels, Ubelgiji, Mei 20, 2025. (Umoja wa Ulaya/kupitia Xinhua)
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer amesema London na washirika wake wako pamoja katika kutunga "mpango unaofaa" wa kurejesha usafirishaji wa meli kwenye mlango bahari huo lakini akifafanua kwamba mpango huo "hautakuwa na pia haujadhaniwa hata kidogo kuwa jukumu la NATO."
Msimamo huo wenye tahadhari unakuja katika hali ya kutokea msuguano wazi na Washington. Hivi karibuni Trump aliikosoa Uingereza kwenye mahojiano ya jarida la Financial Times, akisema London "haikutaka kuja" ilipoombwa msaada kwa mara ya kwanza na ilitoa meli tu baada ya "uwezo wa hatari" kupunguzwa.
Wachambuzi wanasema shinikizo hilo la Marekani huenda lina kusudi la kuhimiza juhudi zaidi za washirika wa Ulaya za kushiriki kwenye vita hivyo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



