Lugha Nyingine
Kenya yafanya semina kutangaza teknolojia ya Juncao ya China katika mifumo ya chakula
Semina ya kutangaza matumizi ya teknolojia ya Juncao ya China katika mifumo ya chakula, kuondokana na umasikini na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi imefunguliwa jana Jumanne katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, na kuwaleta pamoja watunga sera, wanasayansi, wakulima na wajasiriamali.
Semina hiyo ya siku tatu imeandaliwa na Wizara ya Maendeleo ya Kilimo na Mifugo ya Kenya, Kitengo cha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) katika Idara ya Masuala ya Uchumi na Jamii ya Umoja wa Mataifa (UNDESA), na Chuo Kikuu cha Kilimo na Misitu cha Fujian cha China.
Mkuu wa Tawi la Mikakati ya Kitaifa na Ujengaji Uwezo katika Kitengo cha UNDESA, Amson Sibanda amesema, itakapotumika kwa kiwango kikubwa, teknolojia hiyo ya Juncao itaongeza usalama wa chakula na uhimilivu wa athari za mabadiliko ya tabianchi huku ikibadilisha maisha nchini Kenya.
Amesema teknolojia hiyo, iliyovumbuliwa na wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Kilimo na Misitu cha Fujian, imekuwa mfano wa ushirikiano wa Kusini na Kusini.
Naibu mkurugenzi wa Kituo cha Uhandisi na Utafiti wa Teknolojia ya Juncao cha China, Lin Dongmen amesema, matumizi ya teknolojia hiyo yana fursa ya kubadili mifumo ya kilimo na chakula na kuleta uhai mpya katika hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na urejeshaji wa mifumo ya ikolojia nchini Kenya.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



