Lugha Nyingine
Israel yasema imewaua kiongozi wa juu wa usalama wa Iran na kamanda wa Basij wa Iran

Picha hii iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Machi 17, 2026 ikimwonesha Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu (katikati) akizungumza kwa simu. (Xinhua)
JERUSALEM - Vikosi vya Ulinzi vya Jeshi la Israel vimesema jana Jumanne kwamba vilifanya mashambulizi ya anga ya kulenga kwa usahihi mjini Tehran, na kumuua Gholamreza Soleimani, kamanda wa kikosi cha kujitolea cha Basij cha Iran, na Ali Larijani, katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran.
Larijani anaelezwa kuwa mtu muhimu wa kufanya maamuzi nchini Iran kufuatia kuuawa kwa Kiongozi Mkuu Ali Khamenei Februari 28.
Kwa kurejelea vyanzo vya habari vya kiusalama, Kituo cha Habari cha Kan TV kinachomilikiwa na serikali ya Israel na vyombo vingine vya habari vimeripoti kwamba mashambulizi hayo pia yalimlenga Akram al-Ajouri, mkuu wa tawi la kijeshi la kundi la Islamic Jihad, ambaye inaaminika kuwa ameuawa
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel imetoa picha inayomuonesha Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu akizungumza kwa simu, inayodai kuwa "alikuwa akitoa amri ya kuwaua maafisa waandamizi wa utawala wa Iran."
Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran limethibitisha jana Jumanne kwamba katibu wake Ali Larijani ameuawa, vyombo vya habari vya Iran vimeripoti.

Picha hii ya kumbukumbu iliyopigwa Novemba 15, 2024 ikimwonesha Ali Larijani akitoa hotuba mjini Beirut, Lebanon. (Xinhua)

Picha hii ya kumbukumbu iliyopigwa Februari 10, 2026 ikimwonesha Ali Larijani, katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, akifanyiwa mahojiano na Oman TV mjini Muscat, Oman. (Oman TV/kupitia Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



