Lugha Nyingine
Uganda yawaleta tena faru kwenye bonde la Kidepo baada ya miaka 40
KAMPALA – Jana Jumanne Uganda imeanzisha operesheni ya kuhamisha kwa kipindi kipindi faru weupe wa kusini hadi kwenye Hifadhi ya Taifa ya Bonde la Kidepo kaskazini mashariki mwa nchi, ikimaanisha kurudi tena kwa wanyama wa spishi hiyo baada ya miaka zaidi ya 40 ya kutoweka kutoka eneo hilo.
Mamlaka ya Wanyamapori ya Uganda (UWA) imesema katika taarifa kwamba faru wawili wa kwanza wamehamishwa kwa mafanikio kutoka Hifadhi ya Faru ya Ziwa katikati mwa Uganda.
"Uhamishaji wa faru hawa ni hatua ya kwanza katika kuirejesha spishi ambayo hapo awali iliunda sehemu ya urithi wa mazingira ya asili ya mbuga hiyo," amesema James Musinguzi, mkurugenzi mtendaji wa UWA, akiongeza kuwa faru wengi zaidi wataletwa ili kujenga upya idadi ya wanyama pori wanaoweza kuishi na kustawi hapo.
Faru waliangamizwa kutokana na ujangili mkubwa na ukosefu wa usalama mwishoni mwa miaka ya 1970 na mwanzoni mwa miaka ya 1980, na faru wa mwisho katika mbuga hiyo aliuawa mwaka 1983 katika Bonde la Narus, UWA imeeleza katika taarifa yake hiyo.
Habari zimesema kupelekwa tena huko kwa faru ni sehemu moja ya Mkakati wa Kitaifa wa Uhifadhi wa Faru wa Uganda ili kurejesha idadi ya faru ndani ya kiwango chao cha kihistoria na kuimarisha juhudi za kuwalinda kwa muda mrefu.
Urejeshaji wa faru wa Uganda ulianza mwaka 2005 huko Ziwa. Uagizaji wa hivi karibuni wa faru wanane kutoka Afrika Kusini umeifanya kazi ya urejeshaji kupanuka hadi kwenye makazi mapya.
Mamlaka zimesema, kwa sasa Uganda ina faru 61.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



