Lugha Nyingine
Waziri Mkuu wa China asisitiza fursa, ushindani wa haki na imani kwa maendeleo katika hali ya kutokuwa na uhakika

Waziri Mkuu wa China Li Qiang akihudhuria hafla ya ufunguzi wa Jukwaa la Maendeleo la China 2026 na kutoa hotuba kuu, mjini Beijing, mji mkuu wa China, Machi 22, 2026. (Xinhua/Yue Yuewei)
BEIJING - Waziri Mkuu wa China Li Qiang amesisitiza kuunda fursa mpya za soko kupitia ufunguaji mlango na maendeleo ya teknolojia, na kushikilia utaratibu wa soko la kimataifa kupitia ushindani mzuri na wa haki.
Pia amesema maendeleo yenye sifa bora na ukuaji tulivu wa uchumi wa China vitaendelea kutoa fursa za maendeleo kwa dunia.
Li ameyasema hayo wakati akitoa hotuba kuu kwenye hafla ya ufunguzi wa Jukwaa la Maendeleo la China 2026 mjini Beijing jana Jumapili, akisema dunia inapitia mabadiliko makubwa na magumu, huku kukiwa na mielekeo mbalimbali ambayo inakuwepo kwa pamoja, kuingiliana, na kugongana.
"Hatua za upande mmoja na kujihami vinazidi kushamiri, huku nguvu zinazotetea ushirikiano na kuhimiza maendeleo zikiendelea kuwa imara zaidi; ukuaji wa uchumi katika sekta za jadi unakabiliwa na matatizo, huku maendeleo katika nyanja zinazoibuka yakizidi kushika kasi; utaratibu wa kimataifa wenye msingi wa sheria umepata uharibifu na mvurugiko mkubwa, huku nchi nyingi zikisukuma mbele kwa bidii mageuzi na maboresho ya usimamizi wa kimataifa; siasa za nguvu ya kimadaraka zinatamalaki kwa vitendo vya kiholela na visivyojali, huku miito ya kushikilia usawa na haki ikizidi kuongezeka," Waziri Mkuu Li amesema.
Waziri Mkuu Li amewaambia wahudhuriaji maoni yake muhimu.
Kwanza, amesema soko limekuwa rasilimali adimu, lakini linaweza kupanuliwa kila mara na pili, amesema, maendeleo bila shaka yanahusisha ushindani, lakini ushindani mzuri na ushirikiano vinaweza kuleta kunufaishana na matokeo yenye ushindi kwa pande zote.
"Tatu, ingawa njia iliyo mbele inabaki kuwa yenye changamoto, mustakabali mzuri uko ndani ya uwezo wa kufikiwa," Waziri Mkuu Li amesema, akisisitiza hitaji la kudumisha kujiamini, kubeba wajibu, na kuchukua hatua madhubuti.
Waziri Mkuu Li amesema mwongozo wa Mpango wa 15 wa maendeleo ya uchumi na jamii ya kitaifa wa Miaka Mitano (2026-2030) si tu unatumika kama mpango mpya ya maendeleo ya China bali pia kama fursa mpya kwa maendeleo duniani.
Amesema China itaweka mkazo zaidi katika kuhimiza maendeleo yenye sifa bora, kujitahidi kudumisha ukuaji tulivu wa uchumi, kuendelea kujenga mazingira mazuri ya biashara, kutekeleza kikamilifu sera ya kuhudumia zinazowekezwa kwa mtaji wa kigeni kwa njia sawa na kampuni za nchini (national treatment), na kuwezesha kampuni kutoka nchi zote kufanya shughuli zao nchini China kwa kujiamini na kufikia nguvu zao bora kamili.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



